Recent-Post

Loliondo Ngoma Nzito, Msako Washika Kasi

Wakati Serikali ikisema uwekaji mipaka katika pori la Loliondo unaendelea vizuri, Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai ameendelea kulalamika kutojulikana walipo viongozi 10, akiwamo mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Ndirango Senge.

Jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alisema kazi inaendelea vizuri na kwa amani na hakuna vurugu tofauti na tukio lililotokea mwishoni mwa wiki kulipotokea mgogoro uliosababisha askari polisi mmoja kuuawa kwa kupigwa mshale na kufariki.

“Hakuna mgogoro wowote kwa sasa,” alisema Mongella.

Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kutokuwa na taarifa za kutojulikana walipo viongozi 10, akiwapo huyo mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro kama zinavyotolewa na mbunge wa Ngorongoro, Shangai.

Wengine wasiojulikana walipo ni madiwani, akiwamo wa Arash, Methew Siloma, Luka Kursas (Oloipiri), Rago Mkeka (Maalon), Moloimet Saingeu (Ololosokwani) na Joel Reson wa Malambo. Pia yumo Simon Nairiamu (Piyaya), Shengena Kille (Olorien Magaiduru), Kijoolu Hakiya na Rebeca Leshoko viti maalum.

Akizungumza na Mwananchi, Shangai alisema wananchi 31 pia wamejeruhiwa. “Naomba kuwe na ushirikishaji katika zoezi hili ili kuondoa migogoro,” alisema.

Wakati Ole Shangai akisema hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo hakupatikana ili kuzungumzia kupotea kwa watu hao pamoja na majeruhi waliotajwa na mbunge wao.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema taarifa za kukamatwa kuhusiana na mgogoro huo na wale wanaohusishwa na mauaji ya polisi zitatolewa muda si mrefu.

“Japokuwa kamatakamata bado inaendelea kwa sababu wanatajana, ila kamanda atatoa taarifa naomba msubiri, ikiwa tayari tutawapata tu,” alisema ofisa huyo.

Chanzo cha mgogoro

Kwa zaidi ya miaka 30 sasa eneo la pori tengefu la Loliondo limekuwa na mgogoro ambao awali uliwahusisha wananchi na kampuni ya uwindaji ya Ortello Business Cooperation (OBC) na mwingine kati ya kampuni ya utalii ya Thomson Safaris na wananchi wa eneo la Sukenya.

Kutokana na migogoro hiyo, Serikali ilitangaza kutenga kilomita 1,500 za mraba ndani ya pori hilo tengefu lenye kilomita za mraba 4,000 ili lihifadhiwe. Uamuzi huo ulitangazwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kagasheki na kuzua mgogoro uliosababisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kuunda kamati ya uchunguzi.

Katika kuutatua mgogoro huo, Bunge nalo liliwahi kuituma kamati kwenda kuuchunguza mgogoro huo lakini haukupata suluhu, hivyo uondoshaji wa wakazi hao ukasitishwa.

Kati ya mwaka 2010 hadi 2016, mgogoro huo uliibuka tena baada ya kutolewa taarifa na wahifadhi kuwa eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 linaendelea kuharibika kutokana na ongezeko la shughuli za ufugaji na za kijamii.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliunda kamati iliyopokea mapendekezo kadhaa kutoka kwa wananchi, wahifadhi na wadau wengine wanaohusika nao iliyokusanya mapendekezo kadhaa, likiwamo la kuanzisha Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) au kuanzisha mamlaka kamili ya uhifadhi wa eneo hilo ambayo itaihusisha Serikali na jamii.

Hata hivyo, Februari 14 baada ya mjadala kuhusu usimamizi wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali ilieleza mpango wa kutenga eneo la kilomita 1,500 za mraba na kilomita 2,500 zikibaki kwa wananchi.

Uamuzi huo ulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu, Majaliwa aliyefafanua kuwa lengo ni kulihifadhi eneo hilo ambalo ni muhimu kwa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti, kwani ndilo pekee lenye vyanzo vya maji na mazalia ya wanyama.

Hata hivyo, wananchi wa Loliondo wakiongozwa na madiwani wao, wameeendelea kupinga kutengwa kwa eneo hilo kwa madai kuwa wanalitegemea kwa malisho ya mifugo na maji.

Katika kuhakikisha linahifadhiwa, Juni 7 Serikali ilipeleka wataalam na vyombo vya dola kwenda kuweka mipaka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mkoani Arusha, Dk Elifuraha Laltaika ambaye ni mkazi wa Ngorongoro, alisema cha msingi kwa sasa ni kutafuta maridhiano ya pande hizo mbili.

“Tunataka maridhiano, waliokamatwa basi taratibu za kisheria zifuatwe ili waachiwe tuumalize huu mgogoro,” alisema.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa alitaka yawepo majadiliano katika uwekaji wa mipaka hiyo kwani eneo hilo ni muhimu kwa pande zote mbili.

“Wananchi wa Loliondo sio wavamizi katika eneo hilo ndio sababu tunaomba majadiliano,” alisema.

Hali ya Ngorongoro

Wakati hali ikiwa hivyo upande wa Loliondo, huko Ngorongoro zaidi ya wananchi 290 wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro wameridhia kuyahama makazi yao kwenda Kijiji cha Msomera kilichopo Handeni mkoani Tanga.

Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella alisema hadi jana, kaya 290 zilikuwa zimejiandikisha ili kuhama na tayari kaya 20 ziliondoka jana kuelekea eneo hilo.

“Miundombinu inazidi kuimarishwa, nyumba 103 ziko tayari na kesho (leo), tunaanza awamu ya kwanza ya kupeleka mifugo, kuhamisha mali na wao wenyewe kuhama, tumeshajitayarisha kwa utekelezahi wa suala hilo,” alisema Mongella.

 

Post a Comment

0 Comments