Mbio Za Baiskeli Kilimanjaro Kusaidia Sekta Ya Afya


 Raia wa Uholanzi zaidi ya 40 wameanzisha mbio za baiskeli kuzunguka mlima Kilimanjaro kilometa 400 kwa ajili ya kuchangisha fedha kusaidia sekta ya afya nchini.

Mbio hizo za baiskeli zijulikanazo kwa jina la ‘Africa Classic’ zimeratibiwa na Shirika la Amref Netherlands kwa kushirikiana na Amref Tanzania na zinalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia huduma za afya.

Akizungumza leo Jumapili Juni 12, 2022 katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya Amref Health Africa, Anthony Chamungwana amesema mbio hizo za kuendesha baiskeli zilianza rasmi mwaka jana ambapo wamekuwa wakifanya kila mwaka kwa ajili ya kuchangisha fedha kusaidia sekta ya Afya Tanzania na mafanikio makubwa yameonekana.

"Ni miaka miwili tu hatukufanya kutokana na janga la Uviko-19 ila tunashukuru kwa sasa tunaendelea kufanya hivyo na zoezi hili limeleta mafanikio makubwa kwani limesaidia kuboresha sekta ya Afya na kukuza usimamizi katika maeneo mbalimbali "amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Amref Tanzania, Gaspar Jonah amesema kuwa fedha hizo baada ya kuchangishwa na wafadhili hao hutumwa katika shirika hilo kwa ajili ya shughuli za utekelezaji katika maswala ya Afya ambapo Amref Tanzania ni miongoni mwa nchi inayonufaika kwa mbio hizo ambazo wachangiaji kutoka Uholanzi huchangia kila mwaka.

Amesema kuwa, mbio hizo ni awamu ya kwanza ambapo wakitoka hao watakuja wengine awamu ya pili lengo kuhakikisha wanachangisha fedha hizo na kuweza kusaidia maswala mbalimbali katika sekta ya Afya.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jairy Khanga amesema kuwa, swala hilo linalofanywa na  raia  hao wa Uholanzi  ni jambo kubwa kwani linasaidia kutatua changamoto za afya nchini.

"Naweza nikasema ujio wa wageni hawa ni matokeo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza Royal Tour ambapo imechangia sana kurudisha wageni wetu baada ya kutokea kwa janga la Uviko-109 kwani mambo mengi sana yamefunguka kwa sasa."amesema Dk Khanga.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments