Recent-Post

Membe atolea ufafanuzi kauli ya Nape

Wiki moja baada ya mwanasiasa nguli nchini, Bernard Membe kurejea rasmi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu alipofukuzwa mwaka 2020, hatimaye ameeleza kuhusu kauli iliyozua utata iliyotolewa siku ya kukapokewa kwake.


Mei 29 mwaka huu Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje ya Nchi alikaribishwa tena ndani ya CCM baada ya miaka miwili aliyoishi nje ya chama hicho, akihamia ACT-Wazalendo na baadaye kutangaza kuachana nacho na kubaki kuwa mshauri wa kisiasa.

Wakati wa ukaribisho wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alitoa kauli kuwa, "Bahari imetulia, Mwenyezi Mungu ameamua ugomvi, basi baki nyumbani tusonge mbele pamoja".

Kauli hiyo iliibua mitazamo tofauti kutoka kwa baadhi ya wananchi wakitamani kujua ugomvi uliomalizwa na Mungu ni upi, huku tafsiri za baadhi yao zikijielekeza kwenye ugomvi wa kufukuzwa kwake CCM?

Ingawa kufukuzwa kwa Membe ndani ya CCM kulitokana na kile Kamati Kuu ya chama hicho ilichokieleza kuwa ni mwenendo wa kujirudia makosa na licha ya kupewa adhabu nyingine lakini hakujirekebisha.

"Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake (Membe) ndani ya chama zinaonyesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha lakini imeonekana sivyo," alisema aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, Februari 28, 2020.

Akifafanua kuhusu kauli ya Mungu ameumaliza ugomvi, Membe alisema ililenga kuwaeleza wananchi wa tarafa ya Rondo aliokuwa na ugomvi nao kwamba sasa umemalizika.

Alisema kufukuzwa kwake ndani ya CCM kuliibua hasira miongoni mwa wananchi, hatua ambayo ilisababisha katika moja ya mkutano wa Nape kuhudhuriwa na watu 12 pekee.

"Kwa sababu watu walikuwa na hasira na wakabishana pale .... Mimi mwenyewe sikuwepo. Nilipata tabu sana kama mbobevu, kama mataafu, kama mtu ambaye nilimshabikia Nape Nnauye.

"Sasa tumekwenda na hiyo misuguano hadi niliporejea CCM na Nape alikuwa miongoni mwa viongozi ndani ya chama waliokuwa wanakuja kila mwezi kuniomba nirejee CCM. Nikarejea CCM," alisema

Baada ya kurejea CCM, alisema alizungumza na wananchi na kuwaeleza kuwa "yaliyopita si ndwele tugange yajayo" na kusisitiza kuwa mtafaruku ya yao na Nape umalizike

"Nilimtaka Nape alieleze hilo, sasa Nape ni msomi na mwanasiasa, akaliweka kwa lugha aliyoliweka. Kwa hiyo wananchi wa Rondo kauli ya Nape ni ya kueleza kwamba mgogoro wa wananchi wa Rondo na mbunge ambao walikuwa nao sasa umekwisha hiyo ndiyo tafsiri tuliyoipata," alisema

Miaka miwili akiwa nje ya CCM, Membe aligombea urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo alichojiunga nacho Julai 15, 2020 miezi kadhaa baada ya kufukuzwa CCM.

Post a Comment

0 Comments