MJI MPYA IKUNGI KUWAKAMA LONDON, DC AWAALIKA WAWEKEZAJI

Mwonekano wa mji mpya wa Wilaya ya Ikungi.
Mwonekano wa mji mpya wa Wilaya ya Ikungi.

Mwonekano wa mji mpya wa Wilaya ya Ikungi.
Mwonekano wa mji mpya wa Wilaya ya Ikungi. 

 Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeanza mkakati wa ujenzi wa mji mpya wa kisasa ambapo tayari serikali imetoa Sh.600 milioni kupitia Mpango wa Kupanga, Kupima na Kimilikisha Ardhi (KKK). 

Afisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Ikungi, Ambrose Ngonyani, akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, alisema mji huo mpya utajengwa eneo la Unyahati katika kijiji cha Muungano barabara kuu ya Singida-Dodoma. 

"Mji huu mpya ambao tayari viwanja vinepimwa na kuanza kuuzwa kwa wanaohitaji, utakuwa na viwanja vya makazi, hoteli za kisasa, shule, hospitali, vituo vya mafuta na mahitaji yote ya msingi kwa binadamu," alisema. 

Ngonyani alisema hatua iliyoanza ni ilikuwa ni kulipa fidia na baadaye kulipanga, kulipima kuandaa miundombinu ya maji,umeme na barabara ambapo kuna viwanja 1,000 ambavyo vinaendelea kuuzwa. 

Alisema sababu za kuanzisha mji mpya wa kisasa ni kutokana na udumavu wa mji wa Ikungi ambao ndio makao makuu ya wilaya wa sasa ambao hauwezi kufanya chochote na hakuna viwanja vilivyopimwa. 

Ngonyani alitaja sababu nyingine iliyosababisha kuanzisha mji mpya ni ongezeko la uwekezaji katika Wilaya ya Ikungi hasa baada ya kugundulika kwa madini ya dhahabu katika kata ya Mang'onyi. 

Alisema matarajio ya serikali baada ya kuanzisha mji mpya ni kupata mapato yatakayotokana na ardhi na kuwa na miliki za ardhi salama hali ambayo italeta na kuongeza uwekezaji kwa kasi katika wilaya hiyo.

 Ngonyani aliongeza kuwa ujenzi wa mji mpya wa kisasa unatarajia kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa ambapo watu walionunua viwanja wamepewa muda huo kuviendeleza. 

Naye Mkuu wa Wilaya Ikungi, Jerry Muro, ametoa wito kuwakaribisha wananchi,wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja wilayani humo kuchangamkia viwanja na uwekezaji. 

Muro alisema serikali imepanga kufanya mji mpya wa Ikungi kuwa kama London ambao utakuwa na mvuto na wa mfano katika wilaya zote za Afrika Mashariki na kati. 

"Wafanyabiashara au wawekezaji watakaokuja kuwekeza Ikungi kamwe hawatajutia zipo fursa nyingi na ni wilaya ambayo ipo barabara kuu inayounganisha katika mkoa na mkoa wilaya na wilaya, nchi na nchi," alisema Muro. 

Kwa upande wao wananchi wa Ikungi waliipongeza serikali chini ya DC Muro,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi,  Justine Kijazi na wakuu wa idara hususani ya Idara ya Ardhi kewa uamuzi wa kuanzisha mji mpya kwani kumekuwa na mikakati mingi ya kuifufua wilaya iweze kuwa na maendeleo. 

Wilaya ya Ikungi ambayo ni mojawapo za wilaya katika Mkoa ilianzishwa 02, Machi, 2012 na aliyekuwa rais kipindi hicho Dk. Jakaya  Kikwete kupitia GN Na. 73 alitangaza kuundwa kwa wilaya hiyo na 03 Mei, 2013 aliyekuwa Waziri Mkuu,  Mizengo  Pinda kupitia GN. Na. 96 alitangaza kuanzishwa rasmi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. 

Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imetokana na Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Halmashauri ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mnamo 01/07/2013. 

Fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Wilaya ya Ikungi ni pamoja na uchimbaji wa dhahabu,kilimo cha alizeti, kilimo cha mpunga,ufugaji nyuki na kilimo cha kotosho ambapo kuna maeneo makubwa sana kwa ajili ya uwekezaji.

Na Thobias Mwanakatwe, Ikungi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments