Mpina aichokonoa tena Serikali

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amemwomba Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson kuunda tume kuchunguza maeneo matatu ambayo yataifanya taasisi hiyo muhimu nchini kukumbukwa kwa maisha yote.

Maeneo hayo ni ucheleweshaji wa ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere (JHPP), kupanda kwa bei ya mafuta na gharama kubwa za mbolea ambazo amedai zinazowaumiza wakulima nchini.

Mpina alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali huku akieleza kuwa maeneo hayo yana shida licha ya sababu mbalimbali zinazoelezwa, vikiwamo vita baina ya Ukraine na Russia.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Mpina kuibua madai kama hayo akielekeza zaidi mashambulizi kwenye wizara hizo mbili (Kilimo na Nishati) ambapo alishawahi kueleza kuwa kuna uzembe na kulindana katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa umeme.

Katika michango yake bungeni, Mpina amekuwa akirudia kuuzungumzia ujenzi wa bwawa hilo akisema uhalisia wake ni tofauti na hali ilivyo. Lakini, madai hayo yalishajibiwa na Waziri wa Nishati, January Makamba ambaye alieleza kwa kina kinachoendelea kwenye mradi huo.

Kwenye maelezo yake Makamba alisema kuchelewa kwa mradi huo kumechangiwa na janga la Uviko-19 lililochelewesha baadhi ya vifaa muhimu vya mkandarasi kuwasili nchini huku mataifa mengi yakisitisha uzalishaji.

Kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta, Makamba alilieza Bunge inatokana na kupaa kwenye soko la dunia hasa wakati huu ambao Russia akiwa mzalishaji namba mbili kuwekewa vikwazo vya kiuchumi kutokana na mgogoro wake na Ukraine.


“Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine tumeathiriwa sana na vita hii. Tunanunua nishati hii kwenye mataifa mengine kwa sababu sisi si wazalishaji, hivyo hatuwezi kujipangia bei na kwetu tunajitahidi sana ukilinganisha na majirani zetu,” alisema Makamba na kuongeza kuwa: “Kuna hatua zingine zaidi za kikodi ambazo Serikali imechukua ikiwemo kuondoa baadhi ya tozo ili kuhakikisha wananchi wanapata nafuu ya nishati hiyo.


“Tutaanzisha mfuko wa kuhimili ukali wa bei za mafuta ambao utasaidia kupunguza makali ya bei ya mafuta kipindi ambacho bei hizo zinaongezeka kwa kiasi kikubwa na mpango huu uko hatua za mwisho kuanzishwa.


Pia, tutaanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati ambao uanzishaji wake unasubiri marekebisho ya kanuni na kuendesha hifadhi mafuta ya kimkakati ili nchi yetu ijihakikishie usalama na unafuu wa bei katika vipindi kama hivi.”


Kwa sasa bei ya petroli kwa Jiji la Dar es Salaam ni Sh2,994 kwa lita huku dizeli ikiwa ni Sh3,131 huku mafuta ya taa yakiwa Sh3,299 bei ambazo ziko chini kulinganisha na nchi jirani za Kenya na Uganda ambako hata upatikanaji wake pia ni wa kusuasua.


Vita vya Russia na Ukraine vilianza Februari 24, mwaka huu hivyo mataifa ya Ulaya na Marekani kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Russia ambayo pia ni mzalishaji mkubwa wa mbolea.


Hata hivyo, jana Mpina alikumbushia kupanda kwa gharama za mbolea akisema nalo liingizwe kwenye uchunguzi huo kwa madai eneo hilo ni tatizo linalowaumiza wananchi wengi wanajihusisha na kilimo.


“Mheshimiwa Spika, naomba kukupa ushauri ambao hutokaa unisahau katika maisha yako. Naomba uunde tume kuchunguza ucheleweshaji wa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, unda tume ichunguze kupanda kwa bei za mafuta na unda tume ichunguze kupanda kwa bei ya mbolea, utakuja kunikumbuka,” alishauri Mpina.


Katika mchango wake, mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi alizungumzia uamuzi wa Serikali kutaka kubadilisha matumizi ya Ranchi ya Kongwa kuwa shamba la alizeti kwamba hauonyeshi umuhimu wa kuwajali wafugaji wanaoyategemea malisho na miundombinu mingine muhimu inayopatikana shambani humo.


Alisema kuna maeneo mengi nchini ikiwamo Mkoa wa Tabora ambako yangeweza kufyekwa na kulimwa mazao ya kimkakati lakini kuing’ang’ania Kongwa ni uamuzi unaopaswa kupingwa na wabunge wote.


Mwezi uliopita Mpina alipoibua hoja ya mbolea alijibiwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyemwambia kama ana chanzo chochote cha kuiwezesha Serikali mbolea ya bei rahisi wizara ipo tayari kumpa mkataba wa tani 400,000 azilete nchini.


Bashe alisema hayo baada ya Mpina kudai mfumuko wa bei ya mbolea ni wa kutengeneza kwa manufaa ya wafanyabiashara na kutaka takwimu za Serikali ziangaliwe kwani, hazina uhalisia.


“Ni hatari kwa mtu ambaye ni mbunge wa muda mrefu aliyewahi kuwa naibu waziri halafu akawa waziri kusimama bungeni na kuzungumza ishu ambayo totally he is misleading the public (anaupotosha umma).


Bei ya mbolea duniani si jambo la kuficha, hata uki-google unazipata. Nimwombe Mheshimiwa Mpina kama ana-source (chanzo) yoyote ya kunipa mbolea ya bei rahisi aje nampa mkataba wa tani 400,000 zote aniletee,” alisema Waziri Bashe.


Hata hivyo, Mpina hakuwahi kujitokeza kujibu lolote kuhusu ofa hiyo hadi jana alipoibuka tena na kuchokonoa jambo hilo.


Maoni ya wabunge wengine


Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby alisema kuna haja ya kuunda tume ya Bunge kuchunguza suala la bei ya mafuta kwa kuwa mfumo wa kuyaagiza kwa pamoja una matatizo tofauti na ilivyo kwenye mbolea ambako alisema hakuna shida kubwa kwani, kabla ya kuanza kutumika ulifanyika utafiti kwanza.


“Mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja ulifanyiwa kazi kabla ya kuanza, waziri alikuwa mjanja kabla ya kuanzisha aliangalia bei ya mbolea duniani, gharama za usafirishaji hadi kufika hapa nchini na faida zake hivyo hakuna shida,” alisema Shabiby.


Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Nustrat Hanje alisema haoni sababu ya kuundwa tume yoyote kwa sababu mambo yote aliyoyaeleza Mpina tayari Serikali imeshachukua hatua kwa kuyashughulikia.


“Mimi sioni haja ya kuundwa kwa tume kwa sababu Serikali imesha-react (eleza) hatua mbalimbali ambazo wamechukua kukabiliana na mambo hayo, tuwape muda waendelee kushughulikia, tukiona imeshindika ndipo Bunge liingilie,” alisema.


Alisema huwezi kuihukumu Serikali kwa kuunda tume wakati imeshasema hatua inazochukua kukabiliana na masuala hayo na zingine tayari zimeleta unafuu.


Katika hoja ya mafuta, alisema Serikali ilishatoa Sh100 bilioni kwa ili kupunguza makali ya bei ya mafuta na tayari mpango huo umeanza kutekelezwa tangu Juni mosi, mwaka huu na hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Geita, alisema utaratibu wa kutenga fedha ni endelevu hadi bei zitakaporudi kawaida.


Kuhusu mbolea, Serikali ilishatangaza mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei yake ikiwamo kuruhusu wawekezaji kujenga viwanda.


Kati ya yanayofanywa katika eneo hili ni ujenzi wa kiwanda kikubwa hapa Nala jijini Dodoma ambacho kinatarajia kuzalisha tani 500,000 kwa mwaka.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments