Naibu waziri: Bei ya Mafuta haijashuka, Rais Samia Kashusha Bei.

Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kushusha bei ya Mafuta nchini ili kuwapatia wananchi nafuu ya maisha kutokana na kupanda kwa gharama za maisha sehemu mbalimbali nchini.

 

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato alipokuwa akitoa salamu kwa wananchi wa wilaya ya Biharamulo wakati wa ziara ya Rais Samia iliyofanyika Mkoani Kagera Juni 8, 2022.

 

Alisema kuwa bei ya mafuta duniani bado haijashuka isipokuwa serikali imeamua kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 ili kupunguza makali ya bei ya mafuta nchini.

 

"Ruzuku hiyo itaendelea kutolewa kila mwezi mpaka pale bei ya mafuta duniani itakaposhuka, lengo ni kuleta nafuu kwenye gharama za maisha ya watanzania hasa wale waishio Vijijini," alisema  Wakili Byabato.

 

Naibu Waziri huyo aliwahakikishia wananchi wa Biharamulo kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuunganisha Mkoa wa Kagera katika umeme wa Gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika, pia serikali itapunguza gharama ya kununua umeme kutoka nchi ya Uganda.

 

Hata hivyo amesema kuwa kwa kuanzia Serikali imefanikiwa kujenga kituo cha kupoza umeme cha Nyakanazi ambacho kinapokea umeme kutoka mradi wa umeme wa Rusumo na kusambaza katika mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani kama Kigoma kupitia wilaya ya Kakonko.

 

 

Wakili Byabato alisema  kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wanaendelea kuwasimamia wakandarasi wa Miradi ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma hiyo muhimu hasa kwa wale wanaoishi Vijijini.

 

Alisema kuwa Serikali imeunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kuwatambua watu wanaopaswa kuunganishiwa umeme kwa gharama ya sh. 27,000 kwani wananchi wengi bado kipato chao ni kidogo bila kujali mahali wanapoishi, iwe Mjini au Kijijini.

 

Mara baada ya kazi ya kuanisha watu wanaostahili kuunganishiwa umeme kwa gharama ya sh. 27,000 itakapokamilika, kuanzia mwaka 2023 wananchi wataunganishiwa Umeme kwa gharama nafuu ya sh. 27,000.

 Na Mwandishi Wetu, Biharamulo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments