NZUNDA AZINDUA MRADI WA UNENEPESHAJI, UZALISHAJI CHAKULA CHA MIFUGO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika kwenye Taasisi ya Mifugo (TALIRI) Kanda ya Mashariki Tanga kwa ajili ya uzinduzi wa Mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu kwa unenepeshaji wa Ng’ombe nchini uliofanyika kwenye ofisi za TALIRI kanda ya Mashariki Jijini Tanga Juni 23, 2022. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akipata maelezo kuhusu namna vijana walivyowezeshwa kutengeneza mradi wa Majani vlVunde (Saileji) yatakayotomika kunenepesha Mifugo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifugo (TALIRI) Kanda ya Mashariki Tanga Dkt. Zabron Nziku alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya uzinduzi wa Mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu kwa unenepeshaji wa Ng’ombe nchini uliofanyika kwenye ofisi za TALIRI Tanga Juni 23, 2022. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akipata maelezo ya namna ya uoteshaji wa malisho ya Mifugo kutoka kwa Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Mifugo (TALIRI) Kanda ya Mashariki Tanga Bw. Walter Mangesho alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya uzinduzi wa Mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu kwa unenepeshaji wa Ng’ombe nchini uliofanyika kwenye ofisi za TALIRI Tanga Juni 23, 2022.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amezidua Mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu kwa unenepeshaji wa Ng’ombe nchini uliofanyika kwenye ofisi za taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) kanda ya Mashariki jijini tanga Juni 23, 2022.

Katika uzinduzi huo, Nzunda alisema kwamba mradi huo ni ushirikiano kati ya Wizara na COSTECH kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa nyama bora ambazo zinakwenda kuwa malighafi kwenye viwanda, lishe bora kwa wananchi, kupunguza pengo la vyakula vya mifugo kwa kutengeneza mashamba makubwa ya utafiti na mashamba darasa ya malisho ili wafugaji waweze kujifunza na kupata maeneo ya kufuga pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji, wasindikaji na wafanyabiashara wa mazao ya Mifugo.

“Nimeona kazi nzuri mnazozifanya hasa kwenye kituo cha unenepeshaji wa Mifugo ya Nyama, ule ni mfano mzuri wa kuigwa, tunataka vituo hivyo viwe vingi zaidi, tuwawezeshe vijana wanaotoka vyuoni mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, tutakuwa tumewatengenezea ajira za kudumu, tutakuwa na uhakika wa kurudisha fedha na watatoa darasa kwa wengine kupitia elimu ya unenepeshaji,”alisema

“Tumeandaa mpango mkubwa wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo, ili tuweze kujenga tija, tuweze kuimarisha huduma za afya ya Mifugo, tuweze kupata masoko ya uhakika ya Mifugo na bidhaa za Mifugo, na kuwa na mfumo imara wa upatikanaji wa masoko na mfumo imara wa upatikanaji wa malisho kwa kuwaruhusu sekta binafsi kushiriki,” aliongeza

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Mifugo (TALIRI), Prof. Erick Komba alisema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo la kusimamia na kufanya tafiti za Mifugo Tanzania Bara, kuibua, kutathimini na kusambaza teknolojia bora za Mifugo.

“Tafiti tunazozifanya ni pamoja na tafiti za malisho, tafiti za vyakula za Mifugo, uzazi wa Mifugo, uzalishaji wa Mifugo na tafiti za mbali (mbegu) za Mifugo ambapo tafiti hizo zinawezeshwa na Serikali Kuu, wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,”alisema

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Kanda ya Mashariki, Tanga, Dkt. Zabron Nziku aliongeza kuwa, mradi huo una thamani ya shilingi milioni 120 na msingi wa mradi huu ni kutengeneza lishe bora ambayo itaweza kusaidia upatikanaji wa nyama bora na yenye bei nafuu kwa walaji.

Uzinduzi wa mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu kwa unenepeshaji wa Ng’ombe Tanzania ulishirikisha wadau mbalimbali ambao ni viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), viongozi Kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, maafisa mifugo kutoka Halmashauri za Mkoa wa Tanga, watengenezaji wa vyakula vya Mifugo, Wanenepeshaji, wafugaji pamoja na wafadhili wa Mradi (COSTECH).

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments