Recent-Post

Polisi Mkoani Mara Wasaka Mabasi Mabovu Yanayopakia Wanafunzi

Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoani Mara limewaonya wamiliki wa shule binafsi kuacha kutumia mabasi mabovu kubeba wanafunzi.

Limetaka magari ya kubeba wanafunzi yawe yenye ubora na kukidhi vigezo vya usalama barabarani.

Onyo hilo limetolewa na mkuu wa kikosi hicho mkoani humo, Mathew Ntakije leo Jumamosi Juni18, 2022 wakati wa ukaguzi wa magari ya kubeba wanafunzi.

Amesema wamebaini  magari mengi yanayotumika kubeba wanafunzi  yalikuwa yakitumika kubeba abiria.

"Tumegundua magari yakishachoka ndio yanaletwa kubeba wanafunzi sasa niwaambie tu wamiliki wa shule kuwa wanafunzi ni kundi moja muhimu sana, linahitahi uangalizi wa hali ya juu hatutasita kuyaondoa barabarani magari yote ambayo hayakidhi vigezo vya usalama barabarani," amesema.

Amesema ukaguzi wa magari ya kubeba  wanafunzi ambao umeanzia  manispaa ya Musoma utafanyika  wilaya zote za Mkoa wa Mara na utakuwa endelevu lengo likiwa ni kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na ubovu wa magari hayo.

Amesema  ukaguzi utakwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa madereva wa magari hayo ambao wataendelea kufuatiliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Mara, Longinus Tibishubwamu amesema usalama wa watoto wakiwemo wanafunzi ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele na jeshi hilo.

"Tumebaini magari yanabeba wanafunzi wengi kuliko uwezo wake, unakuta zaidi ya wanafunzi watatu wanakalia siti moja jambo ambalo ni hatari lakini pia yapo magari mengine mabovu," amesema.

Mmoja wa wamiliki wa shule binafsi mjini Musoma, Selestine Kato amesema  uamuzi wa kufanya ukaguzi unaungwa mkono na wamiliki wa shule na kwamba atakayepatikana na makosa achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

"Ubovu wa gari ni uzembe wa mtu binafsi na isichukuliwe kuwa wamiliki wote wa shule wana magari mabovu,  tunaomba jeshi la polisi lifanye ukaguzi huu mara kwa mara na kutoa elimu pia ili tusijisahau kwani usalama wa wanafunzi ni jambo muhimu sana," amesema Kato.

 

Post a Comment

0 Comments