PROGRAMU YA ROYAL TOUR YAENDELEA KUIFUNGUA TANZANIA

Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani wakati akichangia hoja bajeti ya wizara ya Maliasili na Utalii.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana akiwa na Naibu waziri wa Wizara hiyo Mhe. Marry Masanja wakifuatilia hoja za Wabunge leo June 3, 2022 bungeni Dodoma.

PROGRAMU ya kutangaza vivutio vya utalii ya The Royal Tour imeanza kuleta matunda kwa kuvutia watalii na wawekezaji mbalimbali nchini.

Programu hiyo imewahamasisha wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka katika masoko ya utalii yakiwemo Marekani, Ufaransa na Lithuania waitembelee Tanzania kujifunza na kujionea vivutio vivutio vya utalii vilivyopo kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana alipokuwa akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2022/2023 ambapo amesema wawekezaji kutoka Taifa la Bulgaria wameonesha nia ya kuwekeza Tanzania kwa kujenga hoteli nne (4) zenye hadhi ya nyota tano (5) katika hifadhi za Taifa za Serengeti, Ziwa Manyara na Tarangire; na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Dkt Chana amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi anazozifanya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia programu ya Tanzania – The Royal Tour

“Serikali imesaini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya utalii, biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Jiji la Dallas Marekani. Hatua hii itafungua fursa za usafiri wa anga kwa kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Tanzania hadi Dallas, Marekani na hivyo kuongeza idadi ya wageni nchini”. Alisema Waziri Balozi Dkt Chana.

Waziri Chana ametoa wito kwa Wabunge na Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais za kutangaza utalii na kuvutia uwekezaji kwa maslahi ya Taifa.

Wakichangia hotuba hiyo, baadhi ya Wabunge waliishauri Serikali kuongeza kasi ya kutatua changamoto ya migongano kati ya binadamu  na wanyamapori ambayo inahusisha Hifadhi na makazi ya wananchi, kufanyia kazi maoni ya tume mbalimbali zilizoundwa kwa ajili ya kutatua migogoro iliyopo.

Licha ya kumpongeza Rais kwa juhudi hizo na mchango wake katika sekta ya Utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour, Mbunge wa Ushetu Mhe.Emmanuel Cherehani ameishauri Wizara ya Maliasili na Utalii ihakikishe inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa rasilimali zilizopo ili kuepukana  migogoro iliyopo kati ya hifadhi na wananchi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments