Rais Samia ametuheshimisha sana asema Waziri Bashungwa

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Innocent L.Bashungwa (Mb) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza sera ya elimu bila ada, kujenga miundombinu mbalimbali na kufungua milango ya ajira kwa Watanzania kupitia kada mbalimbali nchini.


"Tunamshukuru sana Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutekeleza sera ya elimu bila ada, ambapo pamoja na mambo mengine,imepelekea watoto ambao walikuwa hawawezi kusoma kutokana na kushindwa kulipiwa ada, kwenda mashuleni.

"Kutokana na ongezeko la wanafunzi kupitia sera hii, uhitaji wa walimu na miundombinu ya madarasa umeongezeka. Katika kukabiliana na changamoto hii, kwa kipindi cha miezi 15 aliyokuwepo madarakani, Rais wetu mpendwa ametuwezesha kujenga madarasa 15,000 kupitia fedha za mkopo wa IMF, na kutupatia kibali cha kuajiri watumishi wa elimu 9,800 na wa afya 7612.

"Aidha, katika mwaka 2020/21 Serikali iliajiri watumishi 23,000 kada ya elimu na afya. Hatua hizi zinazochukuliwa na Mhe. Rais zinastahili kupongezwa sana;

Mheshimiwa Bashungwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 26, 2022 ambapo ametangaza orodha ya majina ya watumishi wapya walioajiriwa kada ya afya na elimu nchini.

Waziri Bashungwa ametangaza majina 16,676 ya watumishi wapya waliopangiwa vituo vya kazi katika Sekta ya Elimu na Afya nchini.

Orodha hiyo inatokana na waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo baada ya Aprili, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa kibali cha ajira kwa kada za Ualimu na Afya, kwa ajili ya kuajiri walimu 9,800 wa shule za msingi na sekondari na wataalam wa afya 7,612.

Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema, baada ya kupata kibali cha ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa tangazo kwa wahitimu mbalimbali wa Ualimu na Kada za Afya, kuwasilisha maombi ya kazi, kupitia mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kuchakata maombi ya ajira, kuanzia Aprili 20 hadi Mei 8,2022.

Amesema, jumla ya maombi 165,948 yakiwemo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya kada za afya ni 42,558, na kada ya Ualimu ni 123,390.

Amesema, kwa upande wa kada za ualimu,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo jumla ya walimu 5,000 wamepangwa shule za msingi na walimu 4,800 Shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu wa shule za msingi na sekondari 261.

Waziri Bashungwa amesema, kwa upande wa kada za Afya,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia 53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments