RC Ampa saa 48 Wakala Pembejeo Kujisalimisha Polisi

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Generali Marco Gaguti ametoa saa 48 kwa mkurugenzi wa kampuni inayosambaza viuatilifu vya korosho vyenye nembo ya makonde kujisalimisha Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Mkuu huyo alisema kuwa mpaka sasa watu saba wameshakamatwa kutoka katika Wilaya za Newala na Tandahimba.

Alisema kuwa mmiliki huyo anapaswa ajisalimishe yeye mwenyewe ili hatua zingine za kisheria ziweze kufanywa kutoka na na pembejeo hizo kukamatwa zikiwa hazikidhi viwango.

 “Watu saba wameshakamatwa kwa kuwa na pembejeo feki ambapo wanne ni kutoka Tandahimba wakiwa na mifuko 500 watatu Newala mifuko 1,600 ambapo taratibu za kisheria bado zinafanyika,” amesema Gaguti.

“Pembejeo tulikamata zina nembo ya Kampuni ya Makonde nimetoa maagizo mmiliki ajisalimishe ndani ya masaa 48 ili atolee maelezo kwanini pembejeo hizo zipo kwenye maeneo yetu wakati zilishapigwa marufuku kwa kukosa viwango na asipofanya hivyo tutamtafuta popote alipo na kumchukulia hatua,” amefafanua Gaguti

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala, Daniel Zenda alisema kuwa ipo michezo michafu inaendelea juu ya pembejeo feki ambapo wamekamata mifuko 1,230 ya pembejeo ambazo ni toleo la 3 za Makonde Sulpher ambazo zinasadikiwa kuwa ni pembejeo feki.

“Tunasema hazina ubora kwa kuwa ni mabonge bonge yaani hata ukipuliza haifiki inakwenda chini ikifika chini inaharibu ardhi na kushusha uzalishaji hii sio sawa,” amesema Zenda.

“Hawa watu wamechomekea, lengo lao sio zuri wakati serikali ikipambana kuongeza uzalishaji wao wanataka kushusha uzalishaji hili jambo sio sawa ndio maana tunafanya ukaguzi na kuwakamata,” amesisitiza Zenda.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments