RC SINGIDA AAGIZA WAKURUGENZI KUSHIRIKI ZIARA ZAKE BILA KUTUMA WAWAKILISHI

Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mkoa wa Singida wametakiwa kuhudhuria ziara zote za mkuu wa mkoa huo za kusikiliza kero za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi bila ya kuwatuma wawakilishi wao.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge leo Juni 28, 2022 baada ya kupata taarifa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba,Mhandisi Michael Matomora hayupo kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Misigiri kilichopo Kata ya Ulemo wilayani Iramba kwa ajili ya kusikiliza kero zao.

"Mkurugenzi yuko wapi, hawa wananchi wakitoa kero nani atazitatua, namwelekeza RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) RC (Mkuu wa Mkoa) ninapofanya ziara wakurugenzi wawepo na kama kuna ruhsa nijulishwe nafasi yake itawakilishwa na mtumishi mwingine," alisema na kuongeza.

"Hapa nina Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) ana kazi nyingi sana, nina Meneja Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA),nina watu wa maji Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wapo hapa ni kwasababu tunataka kero zao wazisikilize moja kwa moja kutoka kwa wananchi," alisema.

Dk.Mahenge alisema yeye ni mwakilishi wa rais hivyo kero za wananchi rais atazipata moja kwa moja kwasababu wananchi wana haki ya kumweleza kero zao.

Alisema kulikuwa na ulazima gani kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ua Iramba kwenda kuhudhuria mkutano wa Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwanini asingetuma mwakilishi kwenda huko ili yeye (DED) ashiriki ziara.

"Marufuku DC (Mkuu wa Wilaya) na nipate maelezo kama hakukuwa na mtu mwingine wa kwenda huko mpaka aende yeye tu, hata aliyemwita alipaswa anieleze mimi Mkuu wa Mkoa kwamba tunajua una ziara lakini tunamwitaji DED tuone kama ni yeye tu ndo anatakiwa aende maana halmashauri ni taasisi," alisema.

Akizungumzia kero ya maji iliyotokewa na wananchi aliigiza Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) mkoani hapa kwamba wiki ijayo wananchi wa kijiji cha Misigiri waanze kupata mara baada ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha kufunga transifoma ili mota za kusukumia maji zianze kufanya kazi.

Kuhusu elimu aliwapongeza wananchi wa Wilaya ya Iramba kwa kuchangia fedha za chakula kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi 76 na za sekondari 25 hatua ambayo imesaidia wilaya hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la Saba na kidato cha nne.

"Msingi wa mwanafunzi kufanya vizuri ni pale tu anapokuwa hana njaa akiwa darasani, nawashukru wananchi wa Iramba kwa kuendelea kuchangia fedha za chakula," alisema.

Aidha,Mkuu wa Mkoa aliwahidi wananchi hao kuwa kero zote walizoziwasilisha serikali itazifanyia kazi. Katika ziara yake RC anaongoza na watalaam wa idara zote za serikali ambao hueleza kazi zilizofanywa na serikali na zinazoendelea kufanyika na kujibu kero za wananchi zinazo husu maeneo yao.

Katika hatua nyingine Dk.Mahenge aliagiza kufanyike uchunguzi baada ya mama mmoja Maria Isaya kudai wajawazito wilayani humo wanatozwa fedha wanapoenda kujifungua ambapo kwa mtoto wa kiume ni Sh.60,000 na mtotowa kike Sh.50,000 na mjamzito anapotakiwa kufanyiwa upasuaji anatakiwa atoe kuanzia Sh. 200,000 hadi 300,000 na huku madai mengine yakiwa ni kujinunulia vifaa vya kujifungulia kwa kutozwa Sh.60,000 ili hali huduma hiyo inatolewa bure na Serikali.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Misigiri kilichopo Kata ya Ulemo wilayani Iramba mkoani humo kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akizungumza na wananchi katika mnada wa Kitukutu ambapo pia Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge alipata fursa ya kuzungumza nao na kupokea kero zao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Sangoma akizungumza kwenye ziara hiyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi (ACP) Lukas Mwakatundu akizungumza na wananchi hao ambapo aliwaomba wafanye shughuli za ujasiriamali kama za kufungua migahawa na hoteli za kulala wageni na vijana kutojiingiza katika vitendo vya wizi katika malori ya mizigo yanayoegeshwa katika eneo la Misingiri jambo litakalo wafanya madereva wa magari hayo kupata muda wa kupumzika na hivyo kupunguza ajali zinazotokea Mlima wa Sekenke kutokana ka kuwa na usingizi.
Mkazi wa Kijiji cha Misigiri akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mkazi wa Misigiri Evalyene Lyanga akizungumzia kero ya maji inayohusu bili kubwa na malipo ya fidia za nyumba zao zinazotakiwa kupisha ujenzi wa stendi ya mabasi.
Mkazi wa Kata ya Ulemo Elinipendo akiuliza swali kuhusu bima ya afya.
Mkuu wa Mkoa ya Singida Dk. Mahenge akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.
Mkazi wa Kijiji cha Misigiri, Rhoda Philipo akizungumzia mama yake mzazi kupotea katika mazingira ya kutatanisha tangu mwaka jana ambapo hadi leo hii hajulikani alipo.
Wananchi wa Kijiji cha Misigiri wakiwa wamejipanga foleni tayari kwa kutoa kero zao kwa mkuu wa mkoa.
Maswali kuhusu Bima ya Afya yakijibiwa.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Bi. Elizabeth Shalua akitoa kero yake.
Mkazi wa Kijiji cha Misigiri, Shelua Gelema akielezea jinsi walivyopata eneo la mnada wa Kitukutu ambapo kuna mkazi mmoja wa eneo hilo amewatishia waondoke kwa kutumia silaha aina ya bastora.
Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Singida, Onesy Mbembe akijibu maswali ya wananchi.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Msama K. Msama akielezea mikakati ya ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments