SERIKALI AWAMU YA SITA IMEONA MBALI KWENYE HILI LA KUCHAKATA GESI NA KUUZA SOKO LA DUNIA

 Kuna hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuzichukua katika kufungua fursa za kukuza uchumi wa Taifa a Tanzania.


Rais Samia kwa nyakati tofauti amekuwa akieleza dhamira aliyonayo ya kuhakikisha nchi ya Tanzania inaendelea kupiga hatua kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo ya rasilimali zilizopo ambazo muumba wa mbingu na nchi ameamua ziwe kwenye taifa hili.

Ni ukweli usiopingika nchi yetu imejaliwa kuwa na kila aina ya rasilimali.Hakika hakuna ubishi Mungu aliamua kutoa upendeleo kwa Watanzania.Rais wetu mpendwa Mama Samia ameona iko haja pamoja na uwepo wa rasilimali za kila aina sasa umefika wakati wa kutumia rasilimali ya gesi asilia kujenga uchumi imara.

Ni ukweli usiopingika Tanzania tunayo gesi asili ya kutosha na kwa mujibu wa Serikali inaeleza wazi kuna futi za ujazo wa gesi asili trilioni 57.54 ambazo zimegundulika kuwepo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kavu na baharini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizipo gesi iliyoko kwenye kina cha bahari ni futi za ujazo trilioni 47 .3 na futi za ujazo trilioni 10.41 ziko kwenye maeneo ya nchi kavu.Ninaposema Tanzania tumejaaliwa kuwa na kila aina ya rasimali unaweza kuona tu kwenye takwimu hizo.

Hapo sijazungumzia madini, sijazungumzia eneo la utalii.ukitaka kujua ninayokwambia tenga muda kisha angalia filamu ya The Royal Tour. Rais Samia amerahisisha kwa kuweka mambo mengi yanayoihusu nchi yetu.

Ngoja nirudi kwenye hili la gesi asili na mkakati wa Serikali ya Awamu wa Sita katika kuanza kuibadili gesi hiyo na kuwa kimiminika(majimaji) ili kuuza kwenye soko la dunia na nyingine itatumika hapa hapa nchini.

Kwa lugha nyepesi na rahisi tunasema gesi hiyo asili itachakatwa na kusafirishwa kwa ajili ya matumizi ya majumbani.Kwa kifupi kabisa huwa wanaita LNG.

Katika kufanikisha mkakati huo wa Serikali tayari mkataba wa awali umeingiwa kati ya Tanzania na kampuni ambazo zitashiriki kikamilifu katika hatua za awali hadi kuhakikisha inaingia kwenye soko la dunia.

Utiwaji saini wa mkataba wa awali umefanyika Ikulu Dodoma na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Samia.Hongera Mama kwa kuendelea kuchukua hatua sahihi za kujenga uchumi wa Taifa hili kwa kutumia nishati ya gesi.

Ukweli ni kwamba Taifa la Tanzania litanufaika kwa kiwango kikubwa na mkataba wa uchakatwaji wa gesi asili kuanza kutumika majumbani na hivyo inakwenda kufungua fursa za kiuchumi

Tunaamini kupitia mradi huo nchi yetu inakwenda kuimarika kiuchumi wa taifa lakini wakati huo huo na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Ndio tunafahamu wapo ambao watanufaika na ajira za moja kwa moja , lakini wapo ambao watanufaika na ajira za muda mfupi.Tunaelezwa katika kuchakata na kusafirisha gesi hiyo asili kutakuwa na ujenzi wa miundombinu katika nchi kavu na baharini.Unaweza kuona ni kiasi gani cha watanzania watahitajika wakati wa ujenzi.Kule ambako mradi huo unapita nako kuna watu ambao watanufaika kwa namna moja ama nyingine.

Ikumbukwe wakati nchi yetu itakapoanza kutumia gesi hiyo asili kujenga uchumi imara wakati huo huo itakuwa inakwenda kuimarisha na kuboresha mazingira ya uoto wa asili.

Tunafahamu hivi sasa kumekuwa na kiwango kikubwa cha matumizi ya kutumia kuni na mkaa kwa ajili ya matumizi ya kupikia lakini gesi hiyo itakapoanza kutumika inakwenda kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.



Kwa lugha ya mjini tunasema mkakati huo wa Serikali unakwenda kuua ndege wawili kwa jiwe moja.Tunakwenda kujenga uchumi imara wa nchi yetu na wakati huo huo tunakwenda kulinda mazingira yetu na kuacha uoto wa asili ukichukua nafasi.

Nani asiyejua namna ambavyo kuni na mkaa zimekuwa chanzo kikubwa cha kuharibu misitu yetu?Wote tunajua. Ni ukweli usiopingika na hapa nisisitize tena kueleza kwenye mchakato huo wa kuchakata gesi asili inakwenda kuongeza ajira itakayotokana na uuzaji wa gesi hiyo ndani na nje ya nchi.

Hiyo itasaidia si tu kuongeza ajira bali na kuongeza fedha za kigeni kutoka nje ya nchi ambazo zitazidi kuimarisha uchumi wa nchi.



Nikiri na naomba nieleze bila kupepesa macho uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mama yetu Samia ni maamuzi sahihi sana wa kutumia rasilimali hii adimu inayopatikani kipekee nchini Tanzania kwa mamilioni ya tani za ujazo na kwa uhakika.

Mkataba huu umekuja wakati sahihi ili kuinua uchumi wa nchi na kusaidia kuliepusha taifa kupoteza fedha nyingi za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika kuagiza gesi hii nje ya nchi ambapo hadi sasa mahitaji ni makubwa.

Jamani Watanzania wenzangu naomba tuelewane na tusikilizane iko hivi mkataba ambao Serikali umeingia na kampuni za uchakataji wa gesi ni sahihi na umekuja wakati muafaka.Kampuni husika ambazo zitafanya kazi hiyo zimeeleza wazi gesi ya Tanzania ina hewa ukaa chache sana ukilinganisha na gesi inayopatikana kwenye nchi nyingine.

Ujue hivi sasa Dunia inaendelea na mikakati ya kupunguza kiwango cha hewa ukaa ambacho kimekuwa kikisababisha madhara makubwa yakiwemo ya mabadiliko ya tabianchi.Hivyo Tanzania kuwa na gesi asili yenye hewa ukaa chache maana yake inafanya mataifa mbalimbali kutumia gesi yetu.

Wakati wa utiwaji saini wa makubaliano ya awali wawakilishi wa kampuni hizo ambazo zitakuwa zikichakata gesi hiyo walisema wamefikia hatua hiyo kutokana na kutambua jitihada za Serikali kutoa kipaumbele kwenye mradi wa LNG.

Pamoja na maelezo mengi ya wawakilishi hao, hawakusita kueleza tangu ugunduzi wa gesi kumekuwepo na majadiliano mbalimbali na sasa ni wakati muafaka wa kuendelea na mchakato huo na mambo yakienda vizuri wana uhakika gesi asili ya Tanzania itachakatwa na kuingia kwenye soko la dunia.

Wawakilishi hao wameongeza kuwa uzuri wa gesi ya Tanzania itakuwa na soko kubwa na sababu ni ile ile hewa ukaa iliyoko ni chache.Binafsi natamani kila mtanzania huko aliko atoe pongezi kwa Rais Samia na Serikali yake ya Awamu ya Sita.Wamekuja na uamuzi sahihi kwa wakati sahihi.

Pamoja na hayo mchakato huo wa kuchakata gesi asili ya Tanzania tena kutoka mkoani Mtwara na lindi inakwenda kuifanya nchi yetu kuwa mdau katika soko la dunia na tunaamini tunayo fursa ya soko la uhakika kwasababu gesi yetu hewa ukaa ni chache.

Tunaambiwa kadri hewa ukaa inapokuwa chache kwenye gesi ndivyo inavyokuwa na soko kubwa.Mungu ameamua hiyo iwe kwetu.Tunataka nini tena.Narudia tena Dunia inahitaji kutumia gesi yenye hewa ukaa chache.

Pamoja na yote hayo Rais Samia alipata nafasi ya kuzungumza na katika maelezo yake alisema kwa muda wote ambao amekuwa akiitumikia Serikali kabla ya kuwa Rais alikuwa akisikia kuhusu mradi huo wa LNG.

Kuna wakati alijaribu kutia mkono kulisukuma jambo hilo lakini haikuwezekana kutokana na mambo yaliyopo, hivyo baada ya kuwa Rais ameamua kuweka mguu chini na kusema hilo lazima liwezekane.

Hivyo alitoa maelekezo ya kutaka mazungumzo yaanze tena na hiyo ilikuwa Aprili mwaka jana na alitoa muda wa miezi sita.Hata hivyo majadiliano hayakuanza kama alivyotarajia na Septemba mwaka jana akafanya mabadiliko ya Waziri wa Nishati na akaelekeza utekelezaji wa jambo hilo.

Sasa anashukuru kwani ameshuhudia tukio hilo la kihistoria la kusainiwa kwa mikataba hiyo.Rais ameeleza hatua mbalimbali za mazungumzo yalivyokuwa yakiendelea na kuna wakati kulikuwa na ugumu wake lakini hatimaye wamefika pazuri.

Rais Samia alieleza kuwa kumekuwepo na miradi mingi ya kimkakati lakini mradi huo wa gesi unaumaalumu kwani utaleta fedha nchini na utaongeza mapato.Hivyo mradi huo ukikamilika utabadilisha taaswira ya uchumi wa nchi yetu.

Akasisitiza yeye anatarajia mazungumzo kuhusu mradi huo yatakamilika Desemba mwaka huu na mradi huo uanze.Lakini akatumia nafasi hiyo kutoa maelekezo ya kusimamiwa kwa maslahi ya nchi wakati wa majadiliano .

Rais amesema huwezi kupata kila kitu unachotaka wakati wa majadiliano , hivyo pande zote mbili ziwe na maelewano na akatumia nafasi hiyo kueleza mradi huo ni wa nchi nzima lakini Lindi na Mtwara ambako unatoka waone manufaa yake.

Aidha akatoa rai majadiliano kuhusu mradi lazima yaoneshe namna ambavyo watanzania watandelezwa kiteknolojia na kielimu ili huko baadae waweze kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo ya gesi na mafuta.

Pia akaeleza mradi mkubwa kama huo unatoa nafasi ya Serikali kuweka mifumo imara itakayosaidia kuulinda. Hakusita kutoa ombi kwa sekta binafsi na watanzania wote kujipanga kwa ajili ya kuhudumia mradi huo ili kuweza kukuza uchumi wa ndani na hatarajii kuona watu wa nje wakija kutoa huduma wakati wa ujenzi wa mradi huo.

Aidha Rais hakusita kueleza kuwa pamoja na kuwekwa kwa saini kuhusu mradi huo lakini ukweli ni kwamba uzalishaji utaanza mwaka 2025.Hivyo amesisitiza umuhimu wa majadiliano kufanyika kama yalivyopangwa kwa kuwa kilichofanyika sasa ni makubaliano ya awali tu.

Pamoja na yote hayo naomba nieleze , Rais Samia amekuwa akionesha kwa vitendo nia yake ya kuona nchi yetu inapiga hatua.Tunayo nafasi ya kila mmoja wetu kumuunga mkono.

Tunafahamu kila ambacho anakifanya moyo wake umetanguliza maslahi mapana ya nchi yetu.Tunaposema Mama anaupiga mwingi lazima tukubali kweli anaupiga mwingi.

Kwenye hili la kufikiria kuanza kuchakata gesi yetu na kuuza nje ya nchi ni jambo lenye nuru na matumaini makubwa, Tanzania inakwenda kukuza na kuimarisha uchumi wake.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments