SHAKA AENDELEA KUCHANJA MBUGA, AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO, ATOA MAELEKEZO KWA VIONGOZI

 KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka, amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Wilaya za Masasi na Newela mkoani Mtwara.


Mbali na kutembelea miradi ya maendeleo, pia Shaka amepata nafasi ya kukutana na wanachama wa CCM, pamoja na wanananchi kwenye vijiji mbalimbali ndani ya Wilaya hizo ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea mikakati ya Serikali katika kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.

Shaka ambaye yupo mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi inayokwenda sambamba na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 pamoja na kukagua Uhai wa Chama kuanzia ngazi ya mashina.

Akiwa wilayani Masasi Shaka amekagua miradi ya maji katika eneo la Chidya ambapo akiwa kwenye mradi huo amepata maelezo ya utekelezaji wa mradi huo na kuelezwa utakamilika kwa wakati uliokusudiwa.

Baada ya kutembelea mradi huo Shaka ametembelea Shule ya Sekondari Chidya ambayo pia inawafunzi wenye mahitaji maalum na akiwa shuleni hapo amepata nafasi ya kusikiliza kero za wanafunzi na kisha kuzitolea maelekezo kwa Serikali ya Mkoa wa Mtwara.

Pia, akiwa shuleni hapo Shaka amesikiliza kero zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum ikiwemo ya uhitaji wa baiskeli za watu wenye ulemavu ili kuwasaidia kuwatoa sehemu moja hadi nyingine. Shaka ameahidi kuwasaidia baiskeli hizo huku akiagiza kero nyingine zote kutafutiwa ufumbuzi.

Katika hatua nyingine Shaka ametembelea Shina la CCM lililopo kwenye Kijiji cha Chiwata kilichopo ndani ya Wilaya ya Masasi na akiwa hapo Wananchi waliopata nafasi ya kuzungumzia changamoto zinazowakabili wameomba kutatuliwa changamoto ya maji, barabara na umeme.

Baada ya kusikiliza changamoto hizo Shaka amewahakikishia Wananchi hao kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itatafuta ufumbuzi wa waharaka na tayari ametoa maelekezo kwa viongozi wa Mkoa wa Mtwara ili wachukue hatua zinazostahili na Wananchi waondokane na kero hizo.

Shaka katika ziara hiyo alitembelea soko la wafanyanyabiashara Masasi na akiwa hapo amepata taarifa za uwepo wa tabaka katika kuwapanga wafanyabiashara,hivyo ametoa maelekezo kwa viongozi wa halmashauri ya Wilaya Masasi kuweka utaratibu mzuri utakaondoa malalamiko.

Wakati huo huo Shaka amefanya ziara wilayani Newala kwa kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero ambapo baadhi ya kero alilazimika kuwasimamisha wakuu wa Idara kutoa ufafanuzi na nyingine alimsimamisha Mkuu wa Mkoa.

Miongoni mwa changamoto nyingi ambazo zimelalamikiwa na Wananchi ni miundombinu mibovu ya barabara,kukosekana kwa maji na umeme kwa baadhi ya vijiji na vitongoji na yote hayo Shaka amewaahidi kupatiwa ufumbuzi wake.
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments