SHAKA ATAKA MAJIBU MRADI WA MAJI ULIOKWAMA NANYUMBU

 Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ameziagiza mamlaka husika kuhakikisha mradi wa maji wa Nandete uliopo wilayani Nanyumbu, Mkoa wa Mtwara unakamilika na kutoa huduma kwa wananchi.


Shaka ameeleza hayo baada ya kupata taarifa kuwa mradi huo hautoi huduma tangu Februari mwaka huu, baada ya pampu na jenereta kuungua.

Akitoa maelekezo kwa viongozi wa serikali na mamlaka husika za Mkoa wa Mtwara, Shaka amesema sababu zilizotolewa kuhusu kutofanya kazi kwa mradi huo haziingii akilini, hivyo alimuagiza mkuu wa Mkoa huo, Marko Gaguti kutumia vyombo mbalimbali ikiwemo TAKUKURU, kutafuta ukweli wa jambo hilo.

"Huu mradi nitabanana mimi na Serikali kuchukua hatua kwa yeyote aliyehusika kukwamisha kwa sababu sijaridhika na majibu ya mradi huu na CCM hatuwezi kukaa na watu wababaishaji." Amesema Shaka alkizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mnanje B.

"Tumekagua mradi wa maji na Ilani ya uchaguzi ya CCM ibara ya 100 inasema tutasimamia usambazaji wa maji mijini na vijiji, ili uchumi ukue lazima tuboreshe huduma za kijamii na miongoni mwao ni huduma ya maji, maji ndio kila kitu.

"Serikali inachukua hatua kadhaa kuondoa changamoto ya maji na katika Mkoa wa Mtwara imeleta Sh. Bilioni 13.9 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji maji. Tunataka ikifika mwaka 2025 utekelezaji wa Ilani iwe imefikia asilimia 95 na moja ya eneo ambalo tunataka kuona linafanikiwa ni maji," alisema Shaka

Akizungumza na wananchi katika Kijiji Cha Mnanje, wilayani Nanyumbu, Shaka alisema anazo taarifa za kutosha za mradi wa maji Nandete, hivyo ametaka kupata majibu kabla ya kuondoka Mkoa wa Mtwara. "

“Nimepokea malalamiko mengi sana kuhusu huu mradi wa maji Nandete. Serikali ya Rais Samia na CCM itasimama na wananchi.

"Hatuwezi kuona watu wachache ambao wanaangalia maslahi yao binafsi wanakwamisha miradi ya maji. Huu mradi wa maji Natende nataka majibu yake na Mkuu wa Mkoa tumia vyombo vyako kupata taarifa na bahati nzuri taarifa zote ninazo. Kuna mambo mengi yamefanyika na hawasemi, kuna mambo mengi yamejificha," amesema Shaka akitoa maelekezo baada ya kutembelea mradi wa maji wa Maratani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Gaguti, alisema amepokea maelekezo hayo na atakwenda kuyafanyia kazi huku akiahidi kutoa majibu kuhusu mradi wa maji Nandete.

Gaguti alisema haiingii akilini kusikia mashine ya kusukuma maji katika mradi huo wa Nandete iliyoharibika Februari mwaka na kuagizwa kutoka Dar es Salaam iwe haijafika kwa muda wote huo.

Awali akitoa maelezo kuhusu mradi wa maji Nandete, Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Simon Mchucha alisema umesimama kutoa huduma Februari mwaka huu baa ya pampu ya kuvuta maji pamoja na jenereta kuungua.

Aidha, alisema walichukua hatua ya kumtaka mkandarasi kununua pampu nyingine ambapo aliagiza kutoka Dar es Salaam lakini hadi sasa haijafika na wanendelea kuisubiri

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Shaka Hamdu Shaka, akikagua mradi wa maji Maratani katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara akiendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Shaka Hamdu Shaka, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara Simon Mchucha kuhusu mradi wa maji Maratani, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Shaka Hamdu Shaka, akizungumza na mmoja wa wananchi waliojitikeza wakati akikagua mradi wa maji Maratani, Kata ya Maratani Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments