Katibu wa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, amesema watanzania wana haki na huru kuchagua chama gani cha kujiunga nacho ikiwa ni matakwa ya katiba ya nchi yetu.
Alisema hayo kwenye mkutano wa shina namba tawi la CCM Likunja, kata ya Likunja wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambako alipokea zaidi ya wanachama 130,kutoka vyama vya upinzani.
“Tuko kwenye maridhiano ya kisiasa ya kufanya siasa safi, siasa za maendeleo na kila mtu yuko huru kwenda Chama chochote anachoona kinamfaa kufanya siasa na kushiriki maendeleo ya nchi yetu. Niliuliza mara mbili mbili je hawa wanakuja ccm kwa hiayari yao? nikaambiwa wameamua wenyewe, nami nawakaribisha sana mmefanya uamuzi wa busara” alisema .
Amesema wanachama hao wa vyama vya upinzani wamekuja wakati muafaka ambapo Rais Samia analitibu taifa kwa maridhiano ya kisiasa na kuimarisha demokrasia nchini.
“ Tunataka siasa za kuvumiliana, siasa za kuheshimiana, siasa za hoja, siasa na kiungwana” alisema huku akiwa ameshika kadi za vyama vya upinzani alivyokabidhiwa.
Shaka alisema vifaa hivyo ni mali ya vyama hivyo kwahiyo atawapelekea wahusika wazipangie matumizi na kamwe hawezi kubaki nazo kwani haitakuwa uungwana.
“Ndugu zangu hizi kadi, bendera, sare na vitabu vya vyama mlikotoka mie nitawarudishia wenyewe ili wajue watazitumiaje” aliuambia mkutano huo wa shina.
Wanachama hao kutoka vyama vya Chadema ,ACT wazalendo na CUF walimkabidhi Shaka, kadi, bendera, sare, hotuba za wenyeviti wao, na katiba za vyama hivyo.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Ruangwa. Erasmus Galosi Libaba alisema wameamua kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na uongozi wa Rais Samia pamoja na maendeleo yanayopatikana wilayani Ruangwa.
Akiwa katika siku yake ya mwisho ya ziara ya mkoa wa Lindi, Shaka alitoa maelekezo kwa mkuu wa wilaya pamoja na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ruangwa kwenda kijiji cha Likunja kuchunguza tuhuma za ufisadi na wizi zinazowakabili viongozi wa eneo hilo.
“Shida yenu hapa naijua, sababu nimeambiwa kabla sijafika. kwahiyo nimemuelekeza mkuu wa wilaya na mwenyekiti wa CCM wilaya waje hapa watume vyombo vya kuchunguza na kiongozi atakayebainika achukuliwe hatua za kinidhamu” alisema na kuongeza
“ Chama hiki si Chama cha mafisadi, wezi na matapeli.. hiyo tusikubali kukaa na viongozi wenye tamaa na ubinafsi wa kuibia wananchi pamoja na kukiuka miiko na maadili ya uongozi. Kwahiyo suala hilo nimeshalitolea maelekezo kwa viongozi wenu wa wilaya niwatoe hofu litafanyiwa kazi kwa haraka” alisema Shaka na kuamsha shangwe na vigelegele miongoni mwa wanachama na wananchi waliojitokeza kumsikiliza.
0 Comments