TUNAIMARISHA MIFUMO ITAKAYOZUIA WANYAMAPORI KUINGIA KATIKA MAKAZI YA WANANCHI-MAJALIWA

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa sasa inaimarisha mifumo itakayozuia wanyamapori wakiwemo tembo kuingia katika makazi ya wananchi ili waweze kuishi kwa amani.

Amesema baada ya Serikali kuimarisha ulinzi na kuzuia uwindaji haramu kwa sasa nchini kuna ongezeko kubwa la wanyama, hivyo inafanya jitihada kuzuia wanyama hao kuingia katika makazi.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 9, 2022) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo Rashidi Shangazi katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alihoji ni kwa kiasi gani Serikali itawahakikishia wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hizo usalama wao ili wasiendelee kupata athari kutokana na uvamizi wa wanyama hao.

“Serikali inawajibu wa kulinda mali na usalama wa raia ndani ya nchi, tayari tumeongeza idadi ya askari wa wanyamapori ambao tunawapeleka kwenye mbuga zilizo karibu na makazi ya watu.”

Amesema jitihada zingine ni pamoja na kuimarisha na kujenga vituo vya kuhifadhia silaha ili kusaidia kuwaondoa wanyama hao na kuwarudisha katika maeneo yao ya hifadhi.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaratibu ujenzi wa vituo 32 vya kuhifadhia silaha kandokando ya maeneo yanayopakana na hifadhi za wanyamapori.

Amesema lengo la Serikali ni kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori hao, hivyo amewahakikishia wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa hifadhi kuwa itahakikisha inaimarisha ulinzi.

“Tutaimarisha ulinzi ili kuzuia wanyamapori kuingia kwenye makazi ya wananchi na kuhakikisha madhara hayo hayajitokezi tena. Tutaendelea kudhibiti maeneo hayo ili wananchi waishi kwa amani.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuimarisha usafiri katika maeneo ya maziwa na bahari kuu ili kuwawezesha Watanzania kufanya biashara na nchi jirani ili kujiongeza kipato. Pia Serikali imejipanga kuimarisha uvuvi kwenye maeneo hayo.

Aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamoga aliyetaka Mbunge kujua Serikali ina mkakati gani wa Serikali kuhakikisha wananchi wanaosafiri kwenye Ziwa Tanganyika na Nyasa wanapewa usafiri mzuri utakaolinda usalama wao na kukuza biashara.

“Waheshimiwa wabunge wote ni mashahidi jitihada zinaendelea za ujenzi wa meli kwenye maeneo hayo na mwanzoni mwa mwaka huu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mkoani Mwanza kushuhudia utiaji saini wa ujenzi wa meli za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.”

Pia, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeshafanya kazi kubwa ya kukarabati meli na vivuko kwenye maeneo yote hayo matatu ya Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa na mbali na ukarabati huo pia bandari zinaendelea kuimarishwa kwenye maeneo yote.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments