Upinzani wageuzwa maficho ya wana CCM

Inaelekea kutimia miaka 30 tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe mwaka 1992. Na iliigharimu nchi miaka 30 chini ya chama kimoja, mwaka 1962 mpaka 1992.

Vinara wa mageuzi waliokuwepo mwaka 1992 hawapo tena. Kuna waliochukuliwa na Mungu, wapo waliopumzika kwa sababu za kiafya na umri.

Mabere Marando hayupo kwenye uso wa jamii kisiasa, Ringo Tenga, Ndimara Tegambwage, Prince Bagenda, si wanasiasa tena. Hata hivyo, kumbukumbu za historia ya mageuzi zinawatambulisha kama watu muhimu waliochochea kabla na waliopokea mageuzi kwa mikono miwili.

Christopher Mtikila, Chifu Abdallah Said Fundikira, Kasanga Tumbo na Kasela Bantu, Shaban Moore, Lifa Chipaka, James Mapalala, Wilfrem Mwakitwange, Seif Sharif, Mwesiga Baregu na wengine, wote ni marehemu. Ila walihusika kuasisi vyama tofauti vya upinzani mwaka 1992.

Edwin Mtei yupo, ila ameshapumzika hekaheka za siasa. Swahiba wake waliyeasisi Chadema, Bob Makani, alishatangulia mbele ya haki, kama Edward Barongo na wengine. John Cheyo yupo na UDP yake tangu mwaka 1992, ingawa sasa ni dhoofu l’hali.

Vijana machachari nyakati za mwanzo za vuguvugu la mageuzi, James Mbatia, Anthony Komu na Freeman Mbowe, hao ndio wapo kwenye uso wa siasa hivi sasa, ingawa kila mmoja na uhusika wake.

Vyama vya upinzani vilivyozaliwa mwaka 1992 na mwanzoni mwa 1993, dhamira ilikuwa moja tu; kuiondoa CCM madarakani na kuchukua dola.

Hoja zilikuwa sera mbaya na uongozi mbaya wa CCM. Hata hivyo, kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995, oksijeni ya vyama vya upinzani iliegemea kwa wahamiaji kutoka CCM.

Katika wapambanaji wa mageuzi mwaka 1992 na 1993 mwanzoni, ni Cheyo peke yake ndiye aliyejitokeza kwa kujiamini katika Uchaguzi Mkuu 1995, uchaguzi mkuu wa kwanza kuhusisha vyama vingi vya siasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Cheyo aligombea urais kupitia UDP. Vyama vingine vya upinzani vilivyosimamisha wagombea urais mwaka 1995 ni Cuf na NCCR Mageuzi ambavyo wagombea wao hawakuwepo nyakati za mwanzo za vuguvugu la mageuzi.

Mgombea wa NCCR-Mageuzi alikuwa Augustino Mrema, aliyekimbilia upinzani kutafuta maficho salama. Cuf, walimsimamisha mwanasiasa msomi, aliyekuwa na umri mdogo kuliko wagombea wote wakati huo, Profesa Ibrahim Lipumba.

Tuweke hoja pamoja

Tangu mwaka 1995, wanasiasa wanaoshindwa kuiona kesho yao njema ndani ya CCM, vyama vya upinzani vimekuwa maficho yao salama, ama kwa kuendeleza safari upande wa pili au kutibu vinyongo vyao.

Mathalan, miezi miwili na siku 23 kufikia uchaguzi, Kigoma Malima alifariki dunia. Malima alikuwa mmoja wa vigogo CCM, alishika nafasi mbalimbali nyeti; Waziri wa Fedha, Waziri wa Elimu, Waziri wa Viwanda na Biashara na kadhalika.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995, Malima alihamia chama cha NRA. Bila shaka ni baada ya kuona giza CCM. Akajiuzulu uwaziri wa Viwanda na Biashara, akauacha ubunge na kujivua uanachama wa CCM. Malima alifikwa na mauti hotelini Uingereza, Agosti 6, 1995. Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 29, 1995.

Kama Malima asingefikwa na mauti, bila shaka alikuwa mgombea mwenye nguvu mno mwaka 1995. Kifo chake kiliacha uchaguzi ukimilikiwa na wagombea wawili; Benjamin Mkapa CCM na Mrema NCCR-Mageuzi.

Mrema alijiunga NCCR-Mageuzi kusaka maficho salama baada ya kuona anavurugwa CCM. Mabere Marando alikuwa Mwenyekiti wa NCCR. Kwa ridhaa yake akajiweka kando. Mrema akawa Mwenyekiti wa chama.

Si mahala pake kuzungumzia majuto ya baadaye ya Marando kwa jinsi alivyovurugana na Mrema, sisi tujikite kwenye mjadala wa jinsi msingi wa kuanzishwa kwa vyama vya upinzani unavyoyumbishwa na wana CCM wanaotafuta maficho salama.

Mwaka 1995, upinzani ulikuwa na nguvu mno. Mrema aliweza kuitikisa CCM si kidogo. Mwaka 2000 na 2005, zilikuwa nyakati za upinzani dhaifu. Mrema baada ya mgogoro wake na Marando NCCR, alipoa. Lipumba akawa kinara wa upinzani.

Ndani ya kitabu, “Nyuma ya Pazia; Chadema Ilivyosalitiwa 2015”, mwandishi Dk Willibrod Slaa amesimulia kuhusu mpango wa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta kugombea urais kupitia Chadema mwaka 2010.

Hata hivyo, Sitta alighairi mpango wake wa kuhamia Chadema, bila shaka ni baada ya kuisoma kesho yake nzuri ndani ya CCM. Ikabidi Chadema wafanye uamuzi wa haraka dakika za mwisho, wakamsimamisha Slaa kuwa mgombea urais.

Kumbe, Sitta alipoona mambo yake si shwari CCM aliamua kusaka maficho salama Chadema, lakini alighairi. Ni kipindi ambacho Sitta alilaumiwa mno na wana CCM kwamba aliporomosha nguvu ya chama hicho ndani ya Bunge.

Mwaka 2015, Chadema walimpokea Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa Tanzania kati ya Desemba 30, 2015 hadi Februari 7, 2008. Oksijeni ya Chadema ikamtegemea Lowassa.

Kwa nini Lowassa alihamia Chadema? Jibu ni moja tu; aliona ndipo kwenye maficho yake salama ya kisiasa baada ya kudhibitiwa jaribio lake la kuingia Ikulu kupitia CCM. Jina la Lowassa lilikatwa kabla ya kuingia Kamati Kuu CCM, katika orodha ya wawania urais mwaka 1995.

Kutoka Agosti 2015 mpaka Machi Mosi, 2019, ilikuwa ni miaka minne kasoro miezi mitano. Lowassa aliona mgogoro wake na CCM ulishakwisha, akaondoka Chadema na kurejea mahali alipopaita nyumbani.

Lowassa alihamia Chadema wakati mmoja na Waziri Mkuu wa Tanzania mwaka 1995-2005, Frederick Sumaye. Mapema mwaka 2020, Sumaye naye aliona Chadema pagumu, bora kurejea nyumbani. Akaifufua kadi yake ya CCM.

Hata aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, mwaka 2020, alihamia ACT-Wazalendo, baada ya kuvurugana na viongozi wa CCM.

Membe alithubutu mpaka kugombea urais kupitia ACT-Wazalendo. Hata hivyo, uhusika wake kwenye uchaguzi ulitoa picha kwamba hakuwa na dhamira ya kweli ya kugombea, ama alifuata jukwaa la kujionesha yupo kisiasa au hesabu zake zilikataa.

Mwisho, mwaka 2022, Membe amerudi CCM. Aliondoka CCM, Mwenyekiti wa chama akiwa Dk John Magufuli, amerejea usukani wa chama ukishikwa na Samia Suluhu Hassan.

Membe alipoondoka, Katibu Mkuu wa CCM alikuwa Dk Bashiru Ally, hivi sasa ni Daniel Chongolo. Kwa kifupi waliosababisha Membe akimbilie ACT-Wazalendo hawapo, ndio maana amerejea nyumbani kwao.

Ni kama Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii wa zamani, aliondoka CCM mwaka 2017, akipishana na msimamo wa chama chake, hasa baada ya tukio la Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu, kupigwa risasi Septemba 7, 2017.

CCM ambayo Nyalandu hakukubaliana nayo ni ya Magufuli. Hivi sasa hayupo, usukani upo kwa Samia, ameona hakuna kikwazo tena, zile tofauti za awali hazipo. Amerejea nyumbani.

Tufunge mjadala

Mwaka 2020, Chadema walipitisha msimamo kuwa wasingepokea na kuwapa nafasi wahamiaji kutoka CCM. Bila shaka ni baada ya kuona wana CCM huvitumia vyama vya upinzani kama maficho ya muda.

Ni sawa na mwanandoa anayechepuka na kuhamisha mapenzi na huduma zake zote kwa mpenzi wa kando, siku mgogoro wa ndoa ukitatuliwa, mchepuko unaachwa solemba.

Kwa historia ya miaka 30 ya vyama vya upinzani, vigogo CCM wamekuwa wakivitumia vyama vya upinzani kama jukwaa la kutibu vinyongo vyao au kulipiza kisasi baada ya kuona hawakutendewa haki CCM.

Ukweli ambao haupingiki ni kuwa wahamiaji kutoka CCM wamekuwa wakisisimua majukwaa ya kisiasa na kuingiza pumzi mpya kwenye vyama vya upinzani.

Kuanzia Mrema na Malima hadi Lowassa na Sumaye. Wapo waliosaidia kujenga mtazamo wa tofauti, kama Membe na Nyalandu. Hata hivyo, nyakati ziliamua tofauti.

Je, uhamiaji huo wa wana CCM una picha gani katika ukuaji wa demokrasia? Jibu ni moja tu; taswira ni chanya, ingawa vyama vya upinzani vina wajibu wa kuongeza umakini katika upokeaji wao.

Makosa ambayo vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya ni kuwaamini mno wahamiaji, wanawapokea, wanawakaribisha mpaka vyumbani, wanaona siri zote, kisha wakishasuluhisha matatizo yao, wanarejea kwenye chama chao. Wanarejea na siri nyingi za ndani.

Balozi Juma Mwapachu alipoona Lowassa ameshindwa urais wala hakusubiri, alirejea CCM haraka, akaomba msamaha. Ni kama Laurence Masha, Chadema walipambana hadi kumfanya mbunge wa Afrika Mashariki, alipogonga ukuta, alirejea CCM.

Ndio, kuna wana CCM huingia upinzani kusaka fursa za uongozi, wakikosa hurejea nyumbani kwao. Kwa miaka 30, vigogo wa CCM wamekuwa wakivitumia vyama vya upinzani kama majukwaa ya kusemea vinyongo vyao, fursa mbadala za kiuongozi na kulipizia kisasi.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments