Viwanja Vitano CCM Kutafuna Mabilioni

Serikali imeomba Bunge liidhinishe Sh10 bilioni kwa ajili ya kukarabati viwanja saba vya michezo, vikiwamo vitano vinavyomilikiwa na CCM, hatua ambayo imepingwa na wadau wa siasa nje ya Bunge, wakihoji matumizi ya fedha za umma kwenye mali binafsi za chama hicho.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Michezo na Sanaa, Waziri wa Wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa aliomba Bunge liidhinishe Sh35.4 bilioni katika mwaka 2022/23, zikiwemo Sh10 bilioni za ukarabati wa viwanja hivyo.

“Kwa hatua ya kwanza (ya ukarabati) vitaanza viwanja saba vilivyopo katika majiji, ambavyo ni Jamhuri (Dodoma), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Sokoine (Mbeya), CCM Kirumba (Mwanza) na Mkwakwani (Tanga), lakini ukarabati huo utavihusisha viwanja vya Uhuru na Benjamina Mkapa jijini Dar es Salaam,” alisema.

Waziri huyo alisema katika hatua ya pili, Serikali itafanya ukarabati wa viwanja vingine kwa kuweka nyasi bandia na majukwaa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Mtwara, Iringa, Tabora na Shinyanga lengo likiwa ni kuhakikisha Tanzania inakidhi vigezo vya kuandaa mashindano ya kimataifa na kikanda.

“Mkakati huu utaiwezesha Tanzaniakufanikisha maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON ambayo tayari Tanzania imependekezwa kwa mwaka 2027 ambayo ni ndoto ya Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuandaa mashindano makubwa ya michezo,” alisema Mchengerwa.

Mpango huo, umekosolewa na baadhi ya vyama vya siasa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

Naibu msemaji wa sekta ya Michezo wa ACT Wazalendo, Vitalis Maembe alisema kabla ya kutumia rasilimali za Serikali katika ukarabati wa viwanja vya CCM, ni vyema vingerudishwe kwa umiliki wa Serikali ili iweze kuvihudumia.

“Walipewa kama walezi kwa sababu kulikuwa na chama kimoja, kama hawawezi kuvirudisha kwa wananchi, wasivikababati kwa fedha zao au watafute pesa za chama ndizo watumie,” alisema Maembe.

Alisema endapo viwanja hivyo vitarudishwa serikalini, wananchi wote watafaidika na uwepo wake.

Kauli kama hizo pia zimetolewa na Mkurugenzi wa Itikadi na Uhusiano wa Kimataifa wa Chadema, John Mrema akisema “ni jambo la ajabu kwa fedha za umma kwenda kukarabati viwanja binafsi. Jambo hilo halikubaliki na linapaswa kupingwa na Bunge.

“Kama CCM imekosa fedha za kukarabati viwanja vyake ikakope. Tukiendekeza tabia hii, mwisho itakuja Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutangaza kukarabati majengo ya CCM.

“Hii haikubaliki na mwakani tutarajie taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Fedha za Serikali) ikieleza hilo,” alisema Mrema.

Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga alisema, ingawa yeye sio mtu wa milki, lakini viwanja hivyo vinaendeshwa kwa makubaliano maalumu.

“Viwanja vinaendeshwa kwa mikataba, hata vyama vingine wangekuwa na viwanja wanaweza kuingia mkataba na kuomba kukarabatiwa,” alisema Lubinga.

Wakati wa kupitisha vifungu, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya alihoji kwa nini kiasi kikubwa cha fedha kitengwe kukarabati viwanja vya CCM wakati academia (vituo vya mafunzo ya michezo) zimetengewa Sh2 bilioni.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul alisema Watanzania wasifikirie vibaya kuhusu Sh10 bilioni zinazokarabati viwanja vya michezo kwa kuwa watakaovitumia si wana CCM pekee bali ni Watanzania wote.

Mpango huo wa Serikali umekuja wakati tayari CCM ilishaweka mkakati wa kuviboresha viwanja hivyo.

Machi 2, 2020 aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema Kamati Kuu ya CCM imeunda kamati ndogo kusimamia mchakato wa kuboresha viwanja vinavyomilikiwa na chama hicho.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Dar es Salaam, Dk Bashiru ambaye sasa ni mbunge wa kuteuliwa, alisema kamati hiyo ndogo iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (mjumbe wa kamati kuu), ilitarajiwa kufanya maboresho katika viwanja 11 nchini.

Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni pamoja na Jamhuri (Morogoro), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Mkwakwani (Tanga), Jamhuri (Dodoma), Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Nangwanda Sijaona (Mtwara), Samora (Iringa), Liti (Singida), Nelson Mandela (Rukwa), Karume (Mara) na Kambarage (Shinyanga).

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments