Watanzania Waaswa Kujitokeza Kwa Wingi Kushudia Kombe La Dunia

Waziri  wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa, ameipongeza Kampuni ya Coca Cola Tanzania kwa kufanikisha ziara ya Kombe Halisi la Dunia la FIFA, huku akisema hafla ya Watanzania kupiga picha na kombe hilo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, itaambatana na uoneshwaji wa Filamu ya Royal Tour.


Royal Tour ni filamu iliyorekodiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikitangaza utalii na vivutio vilivyotapakaa Tanzania na kwamba kutokana na macho ya wadau wa soka Duniani kuelekezwa nchini kutokana na ziara hiyo, basi ni fursa kwa Watanzania kujitokeza sio tu kupiga nalo picha, bali kuona ubunifu wa Rais katika filamu hiyo.

Kombe la Dunia la FIFA limewasili nchini alfajiri ya Mei 31, kabla ya kufanyiwa utambulisho kwa wanahabari katika hafla iliyofanyika Hyatt Regency Hotel na baadaye kupelekwa Ikulu ya Dar es Salaam, lilikopokelewa na Rais Samia – Mtanzania pekee anayeruhusiwa kulishika kwa mujibu wa Sheria za FIFA.

Taji hilo limetua nchini kwa msafara unaoongozwa na Juliano Belleti, beki wa zamani klabu kadhaa Ulaya zikiwamo Villareal, Barcelona (Hispania) na Chelsea ya Uingereza, ambaye alitwaa taji hilo akiwa timu ya taifa ya Brazil katika fainali za Korea Kusini na Japan, mwaka 2002, ambako alikiri furaha kubwa kufika Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utambulisho wa ujio, Waziri Mchengerwa awali alisema kilichofanywa na Coca Cola Tanzania – kufanikisha ujio wa taji hilo ni jambo la kupongezwa, wao kama Serikali wanaunga mkono jitihada hizo na wataitumia ziara hiyo kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Michezo ili kuharakisha ukuaji wake.

“Kesho Juni Mosi itakuwa fursa muhimu kwa Watanzania kupiga nalo picha kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni. Aidha, kutakuwa pia na onyesho filamu ya Royal Tour ya Rais Samia kuanzia saa 11 hadi saa 12. Kwahiyo wito wetu kwa watananazania kujitokeza kwa wingi kuja kuona matukio hayo mawili makubwa,” alisema Mchengerwa.

Tanzania inahitimisha ziara ya taji hilo kwa nchi ambazo hazijafuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, ambapo Afrika ziliteuliwa nchi nne tu, ambazo ni Ethiopia, Kenya na Afrika Kusini, na baada ya hapo, taji hilo litaanza ziara katika mataifa 32 yaliyofuzu fainali za Qatar, zikiwemo tano za Afrika.

Mkurugenzi Mkazi wa Coca Cola Kanda ya Tanzania, Hellen Masumba, alisema subira ya miaka nane kwa Watanzania kusubiri ziara ya zawadi kubwa na ya thamani zaidi duniani ya Kombe la Dunia, hatimaye kiu hiyo imekatwa kwa ziara hiyo, ambayo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2013, na kuoneshwa dimbani CCM Kirumba, Mwanza.

“Nina furaha kuwajuza kuwa taji limetua nchini kwa jitihada za Coca Cola. Hii ni fursa kwa Watanzania kujumuika na wanamichezo hasa soka duniani kote, kwani ujio huu unafuatiliwa kote. Nichukue fursa hii kuwakaribia Benjamin Mkapa kesho ili kupiga nalo picha na kujiwekea kumbukumbu ya kudumu maishani,” alisema Hellen.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa na Balozi wa Kombe la Dunia kutoka (FIFA) mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil Juliano Belletti katika picha ya pamoja na wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Kombe hilo limeletwa na Coca Cola.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Kombe la Dunia  lililo letwa na Coca Cola kutoka kwa Balozi wa Kombe hilo kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil Juliano Belletti katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Mei, 2022
Mwakilishi wa Cocacola Kanda ya Tanzania, Hellen Masumba, akizungumza na baadhi ya viongozi na waandishi wa habari (hawapo pichani)  wa hafla ya utambulisho wa ujio wa Kombe hilo nchini iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, leo May 31-2022.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, (katikati) na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazir, Juliano Balletti (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi WA Coca Cola nchini wakati wa hafla ya utambulisho wa ujio wa Kombe hilo nchini iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, leo May 31-2022. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa na Balozi wa Kombe la Dunia kutoka (FIFA) mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil Juliano Belletti katika picha ya pamoja na wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Kombe hilo limeletwa na Coca Cola.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments