Wizara Kuwatambua Wanaostahili Msamaha Kodi Ya Majengo Kwenye Luku

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza wataalamu wa mifumo ya kodi kupitia upya na kuangalia namna ya kuwasaidia watu wanaostahili msamaha wa kodi ili kuondolewa kwenye tozo za Luku za umeme majumbani.

 Dk Mwigulu amesema katika utaratibu huo, wataangalia namna ya kuwarudishia gharama za kodi kwa wanaostahili msamaha ambao tayari walishatoa kimakosa kwa kuwa mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hutoa nafasi ya kufanya hivyo.

Waziri huyo alikuwa anajibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Ester Maleko ambaye ametaka kujua nini utaratibu wa Serikali katika kutoa msamaha wa kodi ya jengo kwa wale wanaostahili baada ya kodi kuhamishiwa kwenye za luku.

Mbunge huyo amehoji kuhusu waliolipa fedha hizo wakati walistahili kuwa kwenye msamaha lakini kwa sababu zisizo na msingi waliendelea kulipia majengo yao.

Waziri amesema utozaji wa kodi ya majengo kupitia manunuzi ya umeme kwenye mfumo wa Luku hauondoi haki ya msamaha wa kodi ya majengo kwa anayestahili kisheria bali umeongeza ufanisi katika kujiridhisha kuwa muombaji anastahili msamaha ili kuepuka kuwaondolea makato hata wasio stahili.

Amesema utaratibu wa kutoa msamaha wa kodi ya majengo kwa wanaostahili unaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo SURA 289 mhusika anatakiwa kuwasilisha maombi ya msamaha wa kodi ya jengo kwa TRA.

“Baada ya TRA kujiridhisha kuwa muombaji anastahili msamaha kwa mujibu wa matakwa ya Sheria, makato yake katika ununuzi wa umeme kupitia LUKU yatasitishwa, Aidha, Kifungu cha 7(a - l) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289, kimeainisha majengo yaliyosamehewa kulipa kodi ya majengo,” amesema Dk Mwigulu.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments