BILIONI 12 KUTUMIKA KUSAMBAZA UMEME TANGANYIKA.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato 

Wakazi wa Wilaya ya Tanganyika iliyopo katika Mkoa wa Katavi wameipongeza Serikali kwa kutoa fedha ili kufanikisha usambazaji wa umeme katika vijiji 26 vilivyokuwa havina umeme katika Halmashauri hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa hafla ya kukabidhi hundi iliyofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango kwa ajili ya mauzo ya hewa ya ukaa kwa wakazi wa kijiji cha Katuma kilichopo katika wilaya ya Tanganyika Julai 23, 2022.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato aliwaambia wakazi wa Kijiji cha Katuma kwamba Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 24 ili kuwezesha Vijiji ambavyo havina Umeme katika Mkoa wa Katavi vinapata Umeme wa uhakika.

Serikali imetoa shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kusambaza umeme katika Wilaya ya Tanganyika, jambo litakalofanya jumla ya Vijiji 26 vilivyokuwa havina umeme kuwa na umeme wa uhakika.

Wakili Byabato amesema Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kusambaza umeme ili ifikapo mwezi Machi, 2023 vijiji vyote katika wilaya hiyo viwe vimepata umeme.

Mradi huo wa kusambaza umeme katika wilaya ya Tanganyika unafanywa na Kampuni ya ETDCO.

Amesema kuwa hatua itakayofuata baada ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika Vijiji 26 ambavyo havijapata umeme ni kupeleka umeme kwenye ngazi ya vitongoji ili kuwawezesha watu wengi kupata huduma ya umeme.

Kuhusu suala la kufikisha huduma kwa Wananchi, Byabato alisema kuwa Serikali imefungua ofisi ndogo ya TANESCO katika eneo la Ikola ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa watu waishio katika eneo hilo.

Amesema kuwa katika Bajeti iliyoidhinishwa na bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, TANESCO itafungua ofisi ndogo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Tanganyika ikiwemo Mishamo, Mwese na Kasekese ili kurahisisha utoaji wa huduma pindi Umeme utakapowafikia wananchi waishio katika maeneo hayo.

Na Timotheo Mathayo, Katavi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments