Bilioni 25 za Uviko-19 zapelekwa kukamalisha ujenzi Veta

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema kati ya Sh64.9 bilioni ilizopewa wizara hiyo kutoka fedha za Uviko-19, Sh20 bilioni zilitengwa kwa ajili ya umaliziaji wa vyuo 25 vya ufundi vinavyojengwa katika wilaya mbalimbali nchini.

 Kipanga ameyasema hayo leo Jumapili Julai 3, 2022 wakati Kamati ya Bunge ya Bajeti ilipotembelea ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo Stadi (VETA) wilayani Bahi mkoani Dodoma.

“Lakini Sh8.7 bilioni zilikuwa ni kwa ajili ya furniture (samani) ndio hizi unaanza kuziona sasa. Lakini Sh20 bilioni tulipeleka kwa ajili ya kuanza vyuo vya mikoa katika mikoa minne,”amesema.

Kipanga amesema miongoni mwa vyuo ambavyo vilipelekewa fedha hizo ni Chuo cha Bahi ambapo amesema bado kuna changamoto ya umaliziaji wa chuo hicho.

Amesema fedha zilizopelekwa katika chuo hicho zilikuwa Sh695 milioni ambazo hazitaweza kumaliza kazi za nje katika mradi huo na miundombinu ya umeme, maji pamoja na barabara za ndani ya chuo.

Naye Mbunge wa Ole, Juma Hamad Omary ameshauri ujenzi wa majengo mengine ya vyuo ikiwemo madarasa kuwekwa tarazo badala ya tiles ili kuyawezesha kudumu kwa muda mrefu.

Subira Mgalu (Viti Maalum) ameshauri kupitiwa upya kwa mitaala ya vyuo vya VETA hususani ijielekeze katika nchi kufunguka ili iendane na kozi ambazo watazitoa kwenye chuo hicho.

“Utalii ulivyofunguka tuangalie masuala mazima ya hospitality (huduma) namna ya kusaidia mahoteli makubwa yaliyofunguliwa. Badala ya utaratibu wa zamani wa kutoa wafanyakazi katika nchi za jirani tujielekeze katika vyuo vya kati ili kuleta ushindani katika uchumi uliofunguka,”amesema.

Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu ameshauri Serikali kuona uwezekano wa kulipia ada katika elimu ya kati ili watoto wengi wanaojielekeza kwenye vyuo vingi vinavyoendelea kujengwa ili kutengeneza kesho nzuri ya uchumi wa viwanda.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Daniel Sillo ameshauri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutengeneza barabara inayoelekea kwenye chuo hicho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Soko la Ajira, Mipango na Maendeleo wa VETA, George Sambali ambaye amesema kinatarajiwa kuanza kutoa kozi za muda mfupi ambazo zinachukua kati ya miezi mitatu hadi sita, Novemba mwaka huu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments