Dk Mpango: Mikutano, nyaraka za Serikali kwa Kiswahili

Serikali imesema kuanzia sasa nyaraka zote zikiwamo za mikataba na miradi mbalimbali zitakuwa zikiandikwa kwa Kiswahili ili kuhakikisha lugha hiyo inatumika ipasavyo.

Hayo yalisemwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu, tangu Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) lipitishe kila Julai 7 kuiadhimisha.

Dk Mpango alisema nyaraka na mikataba kuandikwa kwa lugha hiyo adhimu itasaidia wananchi kuelewa kila jambo muhimu katika ustawi wa Taifa lao.

Dk Mpango, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan alisema majina ya barabara, mabango, matumizi ya dawa zote na huduma ziandikwe kwa Kiswahili.

Pia, alisema lugha hiyo inapaswa kutumika katika dhifa zote za Taifa, semina, warsha na mijadala ya umma ili kuendelea kukienzi na kukikuza Kiswahili.

Alitaka sheria zote za nchi ambazo bado hazijatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikiana na taasisi za Kiswahili pamoja na wataalamu kuzitafsiri sheria hizo.

Dk Mpango aliziagiza balozi zote zilizopo nje ya nchi kuanzisha vituo vya Kiswahili na kuwataka kuwatumia walimu ambao ni wahitimu wa vyuo hapa nchini na wamesajiliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza).

“Hapa napenda kuagiza balozi zote kuwatumia wataalamu wa lugha ya Kiswahili waliosajiliwa kwenye kanzidata ya Bakita na Bakiza kuchangamkia fursa ya wakalimani wanaotakiwa ofisi ya Umoja wa Afrika,” alisema Dk Mpango.


Salamu za marais

Washiriki walipata wasaa wa kuangalia na kusikiliza video za marais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Msumbiji, Philip Nyusi na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye.

Rais Samia alisema anashukuru Unesco kuitenga siku hiyo kwa kuwa imeipa heshima Tanzania.

Naye Rais Ndayishimiye alisema Kiswahili kimeonyesha wazi ni lugha inayoweza kuileta dunia pamoja, huku shughuli za muziki zikichangia kukisambaza.

“Kupitia Kiswahili, sasa tunazungumza lugha moja, tunasafiri pamoja, tuendelee kuungana pamoja kwa kufanya kazi ili kuifikisha lugha hii mbali,” alisema Rais Ndayishimiye.

Akizungumzia hilo, Rais Nyusi alisema Kiswahili ni moja ya vielelezo vya utamaduni wetu na sio lugha ya mtaani tu, bali inazungumzwa bungeni, kufundishia na kutangazia kwenye redio na televisheni.

Akizungumza vigezo vilivyoifanya Unesco kutangaza Julai 7 ni siku ya Kiswahili, mmoja wa wanakamati kutoka Tanzania, Profesa wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cna Dar es Salaam (UDSM), Alidin Mutembei alisema mojawapo ni kuwa lugha iliyovuka mipaka.


Alichokisema Rais Mwinyi

Juzi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alizitaka nchi wanachama kuona fursa ya kutumia Kiswahili kama nyenzo ya kukuza ajira katika nchi zao.

Dk Mwinyi alitoa kauli hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani visiwani humo, akisema, “hatuna budi sote kuitumia fursa hii kwa mapana zaidi kama ni moja ya fursa za ajira.”

Alisema nchi zote wanachama zione umuhimu wa kutumia fursa hii kwa kukubali kuwatumia wataalamu wa Kiswahili kwa kubadilishana au hata kwa ajira katika shughuli mbalimbali.

Alisema hatua hiyo itakuwa na maana kubwa, mojawapo ni kuonyesha kwamba “hakika tunaithamini, tunaiendeleza na kuipenda lugha yetu ya Kiswahili.”

Nyongeza na Jesse Mikofu (Zanzibar)

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments