GRIDI YA TAIFA KUFIKA MPIMBWE

Wizara ya Nishati imeahidi kuendelea na usimamizi wa miradi ya kuzalisha na kusafirisha umeme nchini ikiwa ni pamoja na kuunganisha Mkoa wa Katavi kwenye Gridi ya Taifa, ifikapo Oktoba 2023.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato alipokuwa anazungumza na Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la Halmashauri hiyo.

Jengo hilo la Ofisi za Halmashauri limezinduliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango Julai 22, 2022.

"Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe inatumia umeme kutoka nchi ya Zambia na umeme huo unapokelewa katika Kijiji cha Katete kilichopo karibu na eneo la Majimoto," amesema Byabato.

Wakili Byabato amesema kuanzia mwezi Julai, 2023 itajengwa njia ya kusafirisha umeme yenye Msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo cha kupoza Umeme cha Inyoga hadi Mpimbwe ili kuwawezesha wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kupata umeme wa Gridi ya Taifa kama itakavyokuwa kwa maeneo mengine ya Mkoa wa Katavi.

Jumla ya Vijiji 27 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe vinapata umeme na Vijiji 4 vilivyobaki vipo kwenye utaratibu wa kupata umeme kabla ya mwaka huu kumalizika, na mkandarasi anaendelea na kazi.

Kuhusu suala la bei ya mafuta, Naibu Waziri amesema Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwa mwezi Julai, 2022 ili kupunguza makali ya bei ya mafuta nchini.

Wakili Byabato amesema kuwa kama ruzuku iliyotolewa na serikali isingekuwepo, Mafuta katika Halmashauri ya Mpimbwe yangeuzwa lita moja ya Petroli kwa sh. 3,674 badala ya 3,397 na mafuta ya dizeli yalitakiwa kuuzwa sh. 3,687 kwa lita moja badala ya sh. 3,320.

Alisisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha watanzania wanapata maisha nafuu katika shughuli mbambali za kimaendeleo, na ndio maana inaendelea kutoa ruzuku kwenye mafuta.

“Serikali pia imetoa shilingi bilioni 2 kuwezesha wajasiliamali wanaoishi Vijijini kujenga Vituo vidogo vya Mafuta kwa njia ya mkopo ili Wananchi wapate Mafuta safi na Salama badala ya kuendelea kununua Mafuta kwenye chupa za Maji kama ilivyozoeleka,” amesema Byabato.
Na Timotheo Mathayo, Katavi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments