Makada 159 wa CCM Moshi Wajitokeza Kuwania Uongozi

Makada 159 wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Hayo yamebainishwa leo Julai 9, 2022 na Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Mjini, Ibrahim Mjanakheri wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu shughuli ya uchukuaji fomu inayoendelea.

Amesema tangu kuanza kwa uchukuaji wa fomu Julai 2 mwaka huu hadi kufikia leo Julai 9, 2022, saa sita mchana, tayari wanachama 159 wamechukua fomu ambapo katika nafasi ya mwenyekiti wa CCM wilaya, wamejitokeza watu 8, wanaume wakiwa 7 na mwanamke mmoja.

Amesema nafasi ya katibu wa siasa na uenezi wa wilaya, wamejitokeza wanachama 12, wanaume wanane na wanawake wanne huku nafasi ya wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya wakiwa wanachama 74.

“Nafasi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa wameshachukua watu 36 na eneo hili wanahitajika watu watatu na wajumbe wa mkutano mkuu mkoa, wanachama 17 wameshachukua fomu na wanahitajika watu wawili. Kwa upande wa halmashauri kuu ya CCM mkoa, wamejitokeza watu 12 na wanahitajika watu wawili katika nafasi hiyo,” amesema Mjanakheri.

Katibu huyo amesema mchakato wa uchukuaji fomu umekuwa wa wazi na kwamba hakuna nafasi ya mtu, hivyo kila mmoja anaruhusiwa kuchukua fomu katika nafasi ambayo anaona anaweza kuitumikia.

“Kila mtu anachukua fomu kulingana na nafasi anayoitaka na alikojipima na kuona anafaa, hakuna mtu ambaye amefika kuchukua fomu, akaambiwa nafasi hii hapana, kila anayefika anapewa fomu kulingana na nafasi aliyotaka,” amesema.

Chanzo Mwananchi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments