Mikutano Ya Rais Samia Yatuliza Nchi

Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa makundi mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa umeelezwa unaituliza nchi.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Machi 19 mwaka jana, alipoapishwa kuwa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam, akichukua nafasi ya Rais John Magufuli aliyefariki dunia siku mbili nyuma.

Katika sehemu ya hotuba yake siku hiyo, Rais Samia alisema, “huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, kufarijiana kuonyesha upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na Utanzania wetu.

“Si wakati wa kutazama yaliyopita, lakini ni wakati wa kutazama yaliyo mbele. Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu. Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali kwa matumaini. Si wakati wa kunyoosheana vidole, bali ni wakati wa kushikana mikono.”

Maneno ya Rais Samia ameendelea kuyatekeleza kwa vitendo na juzi akiwa visiwani Pemba, Zanzibar alikutana na kuzungumza na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani vya ACT Wazalendo, CUF na ADC.

Tayari amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema, kikiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Mazungumzo mara mbili ya Rais Samia na Mbowe Ikulu yamezaa timu za majadiliano baina ya upande wa CCM, Chadema na Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya kuimarisha demokrasia na utawala bora.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema kitendo hicho cha Rais Samia kukutana na makundi mbalimbali, ikiwamo vyama vya kisiasa kinatambulisha aina ya Rais ambaye Watanzania wanaye.

“Rais ni mtu ambaye anapenda maridhiano, anapenda kukaa na makundi mbalimbali ili kuondoa sintofahamu. Mara nyingi amekuwa akisisitiza umuhimu wa kukaa pamoja na kuzungumza.

“Pia, Rais anatekeleza kauli zake ambazo ameahidi katika majukwaa mbalimbali kuanzia akiwa bungeni na majukwaa mengine, ni jambo zuri,” alisema Dk Loisulie na kuongeza kuwa alijipambanua hivyo tangu alipoingia madarakani.

Mwanazuoni huyo alisisitiza mikutano hiyo ya Rais na vyama vya siasa imeleta utulivu wa kisiasa nchini kwa sababu wanasiasa wamepata jukwaa la kuzungumza moja kwa moja kwa mamlaka husika.

Dk Loisulie anaungwa mkono na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji aliyesema Rais Samia anatimiza ahadi yake ya kujenga sura ya maridhiano kwa maana nchi haiwezi kuendeshwa na mtu mmoja.

Alisema tafsiri ya siasa hapa ilipotoshwa katika jamii ya Watanzania wakiaminishwa siasa ni msuguano kati ya kundi moja na jingine, dola kukandamiza wananchi na wananchi nao kupingana na dola.

“Kama mtu wa upinzani, hakuna nafasi ninayoiona nzuri kama kupata fursa ya kukutana na anayekutawala uso kwa uso na ukamweleza asiyopenda kuambiwa hadharani,” alisema Duni.

Alisema kelele za kisiasa zimepungua nchini kwa sababu Rais Samia amefungua milango kwa wanasiasa, wanapata fursa ya kueleza changamoto wanazokutana nazo katika majukumu yao.

“Kinachofuata sasa, atafanya nini baada ya kutusikia na hatua ya kwanza aliyochukua ni kikosi kazi…angalau tumepata jukwaa la kwenda kuwaambia kwa niaba yake na wale wataandika ripoti yao watampelekea,” alisema Duni.

Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo alisema Rais Samia ana nia njema kwa kutoa fursa hiyo kwa vyama vya siasa, alivitaka vyama vya siasa kuweka masilahi ya Taifa mbele kuliko vyama vyao.

“Kama kiongozi wa kisiasa, naona nia njema ya Rais ya kumaliza matatizo ya mabishano na mivutano ya kisiasa katika nchi yetu. Viongozi wa vyama vya siasa waone umuhimu wa kusaidiana na Rais kumaliza haya malalamiko yanayojitokeza katika nchi yetu,” alisema.

Katika mkutano wao na Rais huko Pemba, Doyo alisema walimweleza kuhusu umuhimu wa kuvumiliana katika demokrasia na malalamiko katika chaguzi.

“Tulimweleza Rais kwa nafasi yake ana uwezo wa kuyaondoa (malalamiko) kwa ajili ya kuweka misingi imara na bora na ya kuaminika,” alisema Doyo na kuongeza kuwa, walimweleza Rais kuhusu fursa ya kufanya mikutano ya hadhara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe alisema katika mwaka mmoja wa Rais Samia, siasa za Tanzania zimeingia kwenye ukurasa mpya wa maridhiano na kutoona vyama vya upinzani ni uadui.

“Tunaamini kabisa kwamba hatua anazofuata ni hatua ambazo zimepokewa vizuri kwa sababu katika miaka ya mtangulizi wake, kulikuwa na siasa za kutoelewana kwa sababu ya tofauti za kiitikadi,” alisema Wangwe.

Na  Peter Elias   Dar es Salaam.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments