Naibu Waziri Akagua Vituo Vya Umeme.

Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (Wa Pili Kushoto)Akikagua Kituo Cha Kupoza Umeme Cha Kipawa Jijini Dar es salaam .Wengine Ni Maafisa Kutoka Shirika La Umeme Nchini(Tanesco)
Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (Wa Kwanza Kulia) Akimsikiliza Mmoja Wa Maafisa Wa Tanesco Wakati alipofanya Ziara ya Kutembelea Kituo cha kupoza umeme cha Ras Kilomoni Jijini Dar es Saalam.
Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato(Wa pili kulia) Akikagua  kituo cha kupoza umeme cha Buguruni.Wengine katika Picha Ni Afisa Wa Tanesco
Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato(Wa tatu kushoto )akieleza jambo alipokuwa anakagua kituo cha Kunduchi Wanaomsikiliza ni maafisa kutoka Tanesco
..........................................................
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amekagua Vituo vya kupoza na kukuza Umeme vilivyopo Dar es Salaam kwa ajili ya kufahamu maendeleo ya Vituo hivyo pamoja na kujua hali ya watumishi.

Naibu Waziri amefanya ziara hiyo leo Jumatatu Julai 11, 2022 ambapo ametembelea kituo cha kupoza umeme cha Kipawa, Luguruni, Kunduchi na Ras Kilomoni.

Amesema alitaka kuona Shirika la Umeme nchini (TANESCO) lilivyojipanga kutoa huduma kwa wananchi kupitia Vituo hivyo vya kupoza Umeme.

Pia alilenga kuona jinsi mabadiliko yanayokuja katika Sekta ya Umeme yatakavyopokelewa na Vituo hivyo vya kupoza na kukuza Umeme vilivyopo katika mkoa wa Dar es Salaam.

Byabato amesema kuwa Serikali imetenga Fedha kiasi cha shilingi bilioni 500, fedha ambayo itatumika kuboresha na kuimarisha gridi ya Taifa.

Amesema kuwa Fedha hiyo ni kwa ajili ya kujenga Vituo vya kupoza na kukuza Umeme, ununuzi wa mashine umba na kuboresha njia za kusambaza Umeme nchini.

Serikali inajenga Vituo vipya vya kupoza na kukuza Umeme, pia Vituo hivyo vitapokea Umeme kutoka katika Vituo vya zamani vilivyoboreshwa zaidi.

Naibu Waziri Byabato, amesema wananchi wategemee kuona mabadiliko makubwa katika Sekta ya Nishati ambapo Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wanatumia zaidi ya megawati 600 za umeme.

Mikoa hiyo miwili inatumia robo ya umeme wote unaozalishwa na TANESCO kwa sababu ya kuwepo kwa Viwanda vingi.

Ameeleza kuwa maboresho makubwa ya Miundombinu ya umeme yamejikita katika Mkoa wa Dar es salaam kwa kuwa ndio wenye matumizi makubwa ya Umeme ikilinganishwa na Mikoa mingine.

Serikali imeipatia Wizara ya Nishati sh. 300 billioni kupitia TANESCO kwa ajili ya shughuli nyingine za kuboresha Umeme nchni.

Naibu Waziri amewataka watendaji wanaosimamia ujenzi wa kituo cha kupoza Umeme cha Luguruni kukamilisha mradi huo kwa wakati ili kituo hicho kiweze kutoa huduma kwa maeneo yaliyokusudiwa.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali na watendaji wake kwa kuwa wanafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa kila Sekta nchni ikiwemo ya Nishati.

Amesema malalamiko Ya Umeme nchini Yamepungua Kwa Kiasi Kikubwa na shughuli za kuboresha miundombinu ya Umeme Zinaendelea Kama Ilivyoahidiwa Na Serikali.

Na Timotheo Mathayo, Dar es salaam.
 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments