RAIS SAMIA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA AJALI YA GARI LA SHULE MTWARA

 

Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Brigedia Jenerali Marco Gaguti kufuatia vifo vya watu 10 vilivyotokea katika ajali ya gari.


Ajali hiyo imetokea leo saa moja asubuhi katika eneo la mteremko la Mjimwema, Kata ya Magengeni, kuelekea Mitengo, Mikindani, Mkoani humo.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Nicodemus Simon Katembo, waliopoteza maisha ni watoto 8 (wasichana 5 na wavulana 3) na watu wazima 2 ambao ni dereva na msaidizi wa gari hilo.

Majeruhi ni 19 (wasichana 13 na wanaume 6) ambao wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Ligula mkoani Mtwara kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

ACP Katembo amesema ajali hiyo imehusisha basi dogo la wanafunzi aina ya Hiace lenye namba ya usajili T 207 CTS mali ya shule binafsi ya awali na msingi ya King David iliyopo mkoani humo.

Ajali hiyo imetokana na gari hilo kushindwa kuhimili breki katika mteremko na kupoteza mwelekeo na hivyo kutumbukia kwenye korongo.

Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments