Rombo kunufaika na ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme

Naibu  Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato
Wananchi wa Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro wanatarajia kunufaika na mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme kupitia programu ya Gridi imara itakayowezesha watu kupata Umeme wa uhakika.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Rombo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rombo.

Jiwe la msingi limewekwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango siku ya Jumatatu Julai 18, 2022.

"Jumla ya Vijijini 68 vimefikiwa na huduma ya Umeme katika Wilaya ya Rombo na kati ya Vitongoji 311 ni Vitongoji 31 pekee ambavyo havina Umeme, lakini vipo kwenye mpango wa kupata huduma ya umeme katika mwaka huu"Alisema Byabato

Akizungumza na wananchi wa Rombo, Naibu Waziri wa Nishati, alisema Serikali inatambua umbali uliopo kati ya nyumba moja na nyingine katika masuala ya uunganishaji wa huduma ya Umeme kwenye makazi ya wananchi, jambo ambalo Wizara ya Nishati inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata Umeme bila kujali umbali uliopo”.

Alisema Serikali inaendelea na mipango ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa kujenga Vituo vya kupoza na kukuza Umeme katika maeneo mbambali ya nchi, ikiwemo Wilaya ya Rombo.

 Aliwajulisha Wananchi kuwa njia ya kusafirisha umeme katika Wilaya ya Rombo ni ndefu lakini kupitia fedha iliyotolewa na Serikali kwenye mpango wa Gridi imara kutajengwa kituo cha kupoza Umeme katika eneo la Shimbi Mashariki.

Kituo hicho kitapokea Umeme wenye msongo wa kilovoti 132 kutoka Moshi ili kuwezesha Wananchi wa wilaya hiyo kupata Umeme wa uhakika.


Na Timotheo Mathayo, Rombo  Kilimanjaro.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments