Tamu, chungu siku 1,879 za IGP Sirro


Nafasi ya Simon Sirro kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) imefikia tamati juzi, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumwapisha Camilius Wambura kushika wadhifa huo.

Sirro alitoka kwenye nafasi hiyo ya juu kiuongozi ndani ya Jeshi la Polisi akiwa amefanya kazi kwa siku 1,879 tangu ateuliwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli Mei 28, 2017.

Hata hivyo, Sirro ameteuliwa na kuapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, akifuata nyayo za mtangulizi wake, Ernest Mangu aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya IGP.

Mfahamu IGP mpya aliyesifiwa na Rais Samia

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wadau wa sheria, haki za binadamu, wanasiasa na wanaharakati walisema katika kipindi chake, Sirro, aliyeapishwa jana kushika wadhifa mpya alifanikiwa na kushindwa katika maeneo kadhaa ya kiuongozi.

Mafanikio ya Sirro

“Pamoja na changamoto za hapa na pale, uongozi wa IGP Sirro ulikuwa na ushirikiano na wadau wengine, zikiwamo asasi za kiraia katika maeneo yanayohusu Jeshi la Polisi. Hilo ni eneo ninalodhani alifanya vizuri,” alisema Onesmo Ole Ngurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, (THRDC).

Ngurumwa anataja kasi ya kudhibiti matukio ya kihalifu yaliyokuwepo kabla ya uteuzi wake akisema ni eneo lingine alilofanikiwa Sirro wakati wa uongozi wake.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko alisema Sirro ameondoka kwenye nafasi yake kutokana na mabadiliko ya kiutendaji, huku umma ukikumbuka jinsi alivyokuwa akisisitiza maadili miongoni mwa maofisa, watendaji na askari wa jeshi hilo.

“Kuna siku alikaririwa akiwataka askari polisi kutenda haki katika utendaji wao, wakitambua iko siku wataondoka katika nafasi zao na huenda wanayoyatenda yakawarejea pindi watakapovua sare. Huu ulikuwa ujasiri mkubwa kwa mkuu wa Jeshi la Polisi,” alisema Soko.

Mkurugenzi mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alimpongeza Sirro kwa ujasiri wa kuwataka polisi kufuata sheria wanapowahudumia wananchi, japo alikuwa na udhaifu katika kuwawajibisha askari wanaobainika kukiuka sheria na maadili kazini.

Rais amteua Kingai kuwa DCI

Mafanikio mengine ambayo yamepatikana katika kipindi cha utawala wa Sirro ni kuhakikisha kila kata inakuwa na mkaguzi wa polisi ili kuongeza mkakati wa ulinzi na usalama kwa kusogeza jeshi karibu na wananchi.

Changamoto za kiutendaji

Licha ya kuwapo mafanikio katika uongozi wake, wakosoaji wa utendaji wa Sirro akiwa IGP wanataja tukio la Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi, madai ya vifo vya raia mikononi mwa polisi na matumizi ya mabavu wakati wa ukamataji.

Walidai kuwa, changamoto nyingine ni watuhumiwa kushikiliwa polisi kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani kinyume cha sheria na askari kujimilikisha mali za raia kama simu na kampyuta mpakato kwa kisingizio cha upelelezi.

Kauli na matendo ya kibabe ya baadhi ya viongozi na watendaji wa Jeshi la Polisi, ikiwamo ya “kipigo cha mbwa koko” ni eneo lingine ambalo wakosoaji wanadai aliyekuwa mkuu huyo wa Jeshi la Polisi hakudhibiti.

“Haki jamii na utawala wa sheria haikustawi vya kutosha chini ya uongozi wa Sirro. Polisi walikiuka sheria wakati wa ukamataji, mahojiano na hata kuwashikilia watuhumiwa kipindi kirefu nje ya mamlaka yao kisheria,” alisema Dk Kijo-Bisimba, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Alitaja kasoro nyingine ni Sirro kushindwa kuondoa picha hasi ya Jeshi la Polisi kuonekana kwa maneno na vitendo kujihusisha na siasa kwa kuegemea upande wa chama tawala.

“Kuna wakati aliongea kwa kukosa weledi, hasa pale polisi wanapopata madhila. Mfano ni kauli yake kuwa wazazi wasizae watoto kama Hamza wakati wa tukio la mauaji ya askari polisi Dar es Salaam. Wazazi wa Hamza hawakumtuma kufanya uhalifu ule. Ile kauli haikuwa ya weledi,” alisema Dk Kijo-Bisimba.

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga alitaja kulegalega kwa Polisi Jamii kuwa ni miongoni mwa madhaifu aliyoonyesha Sirro kipindi cha uongozi wake, hali iliyopunguza ushiriki wa hiari wa wananchi katika vita dhidi ya vitendo vya uhalifu.

“Mauaji na vifo vya raia wakiwa mikononi mwa polisi ilikuwa ni udhaifu mkubwa wa Sirro kwa sababu hakujitokeza kukemea wala kuchukua hatua kwa wepesi dhidi ya askari wake waliotuhumiwa kuhusika,” alisema Anna.

Kuhusu maboresho, Ole Ngurumwa alisema kiongozi huyo alishindwa kulifanya Jeshi la Polisi kuwa na utendaji wa kisasa unaojali, kulinda na kutoa haki kwa raia katika kipindi hiki cha kukua kwa demokrasia, haki za binadamu na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ujumbe kwa IGP mpya

Olengurumwa alisema kuhusu uteuzi wa IGP Wambura, ana imani atatumia uzoefu wake kuleta mabadiliko kwenye jeshi hilo.

“Tunaamini uzoefu wa Wambura unaweza kulifungua Jeshi la Polisi na akafanya mabadiliko yatakayotengeneza taswira chanya kwa ngazi zote. Polisi wanatakiwa kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, hili ni jambo la muhimu kuzingatia,” alisema Ole Ngurumwa.

“Akaondoe hii tabia ya polisi kutumia mabavu, utii wa sheria bila shuruti ndio unapaswa kupewa kipaumbele. Polisi pia, ishirikiane na wadau wengine, mfano watetezi wa haki za binadamu maana wao polisi ndio wana jukumu la kulinda haki za binadamu.”

Hata hivyo, alishauri jeshi hilo lifanyiwe maboresho ya kisheria na kimifumo yatakayoongeza ushirikiano kati yake na wadau wengine.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alishauri wateule wapya kupewa nafasi ili kuona watakachofanya, huku akiishauri polisi kujiepusha na siasa kwa kujikita katika jukumu lao la msingi kisheria na kikatiba la ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

“Wanatakiwa kufanya kazi yao ya uaskari; sio siasa. Wajiepushe na wanasiasa,” alisema.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Gloria Kalabamu alisema licha ya mazuri yaliyopo, uongozi wa Jeshi la Polisi unapaswa kuwachukulia hatua baadhi ya askari wachache wanaotia dosari kutokana na matendo yao.

 Chanzo Mwananchi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments