TCU YAFUNGUA DIRISHA LA KWANZA LA UDAHILI 2022/2023

Katibu Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini, (TCU)  Profesa Charles Kihampa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufunguliwa kwa dirisha la kwanza  la udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023 katika ofisi za Tume hiyo jijini Dar es Salaam leo Julai 8,2022.

 

Na Karama Kenyunko,  Michuzi TV

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la kwanza la udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (shahada ya kwanza) kwa mwaka wa masomo wa 2022/ 2023 huku ikianisha sifa zinazohitajika kwa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu mbali mbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Julai 8, 2022 Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita.

Profesa Kihampa amesema, dirisha hilo limefunguliwa kuanzia leo Julai 8, 2022 hadi Agosti 5,2022.

Amesema,udahili wa kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu wa kidato cha sita; wenye Stashahada (Ordinary Diploma); na waliomaliza programu ya ‘Foundation’ ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Ili kufahamu sifa stahiki za kujiunga na Chuo Kikuu waombaji wameelekezwa kusoma vigezo vilivyopo kwenye vitabu vya muongozo vya TCU huku pia wakitakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wamevichagua na kwamba maelekezo ya jinsi ya kutuma maombi yanayotolewa na vyuo vikuu husika.

Aidha Prof. Kihampa amewapa tahadhari waombaji wote wa shahada ya kwanza ikiwa watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote juu ya udahili kuwasiliana moja kwa moja na vyuo husika ama TCU.

"Tunawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini" amesema Prof. Kihampa.

Amesema masuala muhimu ambayo waombaji wanapaswa kuzingatia ni pamoja na kusoma muongozo wa udahili na kuuelewa, kuingia kwenye tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektoniki na kuwasiliana na vyuo ili kupata taarifa huku pia waombaji wenye vyeti vinavyoyolewa na NECTA au NACTE wakitakiwa kupata idhibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Pia Prof. Kihampa amewaba wanachuo na wananchi kuhudhuria maonyesho ya 17 ya Vyuo vya Elimu ya Juu na Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 18 hadi Julai 23, 2022.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments