Uadilifu Utawezesha Kupata Taarifa Sahihi

Viongozi wa mikoa mbalimbali nchini wamewataka wasimamizi wa sensa ya watu na makazi kuwa waadilifu na kufuata maadili ya kazi yao ili kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana kama ilivyokusudiwa.

Sensa inatarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu na wakufunzi katika mikoa mbalimbali nchini wanaendelea kupatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo kusimamia shughuli hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Baada ya mafunzo hayo kwa wakufunzi, yatafuata mafunzo kwa ajili ya makarani watakaozunguka mitaani kukusanya taarifa za wananchi. Mafunzo hayo yatafanyika kwa siku 21.

Viongozi wa mikoa walitumia fursa hiyo kuwataka makarani na wasimamizi kuzingatia maadili waliyopewa kwa lengo la kutimiza matarajio ya Serikali ya kupata idadi halisi ya Watanzania na taarifa nyingine muhimu.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, Anne Makinda akizungumza na viongozi wa dini, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maofisa wa sensa wa ngazi ya mkoa wa Tanga hivi karibuni, alihimiza viongozi kutochoka kuwahamasisha wananchi kushiriki kwenye shughuli hiyo.

Aliwataja viongozi wa makundi ambayo pia Serikali imewapa kipaumbele katika kufanikisha mchakato wa sensa ya watu na makazi kuwa ni wa madhehebu ya dini, kimila, viongozi wa siasa, viongozi wa wamachinga na waganga wa jadi.

Alitolea mfano wa kundi la wamachinga kuwa zoezi hilo linaona ni muhimu kwa sababu wameandaliwa dodoso maalumu kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ili baadaye awaandalie kadi zitakazowawezesha kuaminika hata katika vyombo vya fedha.

“Kwa mpango huu wa Rais ni wazi kuwa kundi la wamachinga litabeba ajira kubwa ya vijana kwa sababu litakuwa la kuaminika na litaweza kukopesheka kupitia kadi watakazopewa,” alisema Makinda, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge.


Morogoro

Katika mkoa wa Morogoro, aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Martin Shigela ambaye amehamishiwa Mkoa wa Geita, aliwaonya makarani walioteuliwa kwa kazi hiyo kupata mafunzo ya sensa kuwa wasidhani kuchaguliwa kwao ni kwa ajili ya kupata posho tu.

Badala yake aliwataka wafuate mafunzo hayo kwa kufuata kanuni na taratibu za sensa kwa manufaa ya wananchi. Katika mkoa huo, wakufunzi 416 wa sensa wamepata mafunzo hayo.

Shigela alisema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu kuona kama fursa kwao kwa ajili ya kupata fedha (posho) na kuwataka kubadilika na kuweka uzalendo mbele kwa kutekeleza kazi hiyo kwa manufaa ya taifa.

“Haya ni mafunzo maalumu siyo picnic, si sehemu ya kupumzika wala kupata posho. Lazima muweke muda wa kutosha katika mafunzo, sikilizeni kile mnachotakiwa kufanya muda utakapofika, bado muda mchache,” alisisitiza Shigela.

Aliwataka wakufunzi hao kuhakikisha wanatumia siku 21 za mafunzo kuwafundisha makarani katika wilaya zote kama walivyopata wao ili kazi iende vyema.

Katika hatua nyingine, Shigela alisema ni lazima makarani wa sensa watoe taarifa kwa viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa muda kuhusu kaya zitakazohesabiwa kila siku kwa muda wa siku sita baada ya kuanza kwa shughuli ya sensa, Agosti 23.

“Ni muhimu wakati wa kukagua mipaka makarani wakaweka mpango kazi kufahamu ni kaya zipi zitahesabiwa Agosti 23 na 24 hadi siku sita zilizopangwa ili watu ambao hawatahesabiwa Agosti 23 wasifikirie wamerukwa ama kusahaulika.

“Shughuli ya sensa siyo ya siku moja kama kupiga kura, hivyo ni lazima watu wanaokwenda kuhesabiwa wafahamu siku yao ili waweze kwenda katika majukumu ya kutafuta riziki, hili ni jambo la kuzingatiwa sana,” alisema.

Naye Dk Christine Ishengoma (Mbunge Viti Maalumu Mkoa Morogoro) akizungumza katika mafunzo hayo aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuendelea kutoa taarifa kuhusu uzazi bila kusita, kwa kuwa zitasaidia katika kuboresha masuala ya afya ya uzazi na taarifa muhimu kwa jamii.

“Hizi taarifa ni muhimu kwa wanawake wote, tuzitoe bila kuzificha, nafahamu sisi wanawake ni jeshi kubwa na tumekuwa wajasiri wakati wote, hivyo tuondoe woga na tuhamasishe wenzetu,” alisema Ishengoma.


Kilimanjaro

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Willy Machumu amewaonya wasimamizi wa sensa kuwa waadilifu na kufuata maadili ya kazi ili kupatikana taarifa sahihi.

Machumu alitoa rai hiyo wakati akizungumza na wakufunzi wa sensa ngazi ya mkoa, ambapo alisema wanapaswa kuwa na nidhamu ya kazi, utiifu wa maelekezo, kutunza siri na kuhakikisha kunakuwa na usalama wa taarifa watakazozikusanya.

“Ndugu zangu, sensa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na tayari mmepata mafunzo kwa siku 21 ya namna ya kutekeleza jukumu hili muhimu. Sasa niwaase, ninyi ni watumishi wa umma, kaonyesheni uzalendo na kila mmoja akasimame vyema katika nafasi yake ili kutimiza malengo ya Serikali,” alisema Machumu.

Aliongeza kuwa: “Niwasihi katika kazi hii tusifanye mchezo, kwani mkiharibu tutakuwa tumeharibu utaratibu mzima wa sensa kwa mwaka huu 2022 na mnatambua haliwezi kurudiwa tena hadi baada ya miaka 10. Zingatieni umakini na weledi wa kutosha, kufikia malengo ya Serikali.”

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, walisema elimu na hamasa bado vinahitajika katika jamii kwa kuwa katika mafunzo ya vitendo waliyoyafanya, wamebaini changamoto nyingi, ikiwemo hofu ya utoaji wa taarifa za thamani ya majengo na kukosekana kwa namba za vitambulisho vya taifa na anuani za makazi.

Mwalimu Helena Saanane alisema wananchi wengi wanapoulizwa habari za majengo na thamani zake, wanahofia kuzitoa na wengine wakiona taarifa watakazotoa zinahusika na utozwaji wa kodi.

“Tulipokwenda viwandani tulikuta changamoto nyingi, watu wamekuwa wakisita kutoa taarifa kwa usahihi, mfano swali la kumuuliza mtu nyumba yako ina thamani kiasi gani, kwa huku kwetu Kilimanjaro wanashangaa, wanaona sio sawa kuzitaja,” alisema.

Msafiri Msuya alisema: “Wananchi wana hofu ya kutoa taarifa, hasa za majengo, ukimuuliza jengo lake lina thamani gani au habari ya mita za umeme anakuwa na hofu na wengi wanahusisha suala hilo na kodi, lakini pia wengine hawana namba za vitambulisho vya taifa.”

Alishauri uhamasishaji uendelee na vitu ambavyo ni muhimu, ikiwemo vitambulisho na nyaraka nyingine zinazohitajika ziandaliwe kama familia ili karani atakapofika taarifa sahihi zipatikane.


Iringa

Aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Queen Sendiga ambaye sasa amehamishiwa mkoani Rukwa alitumia kitabu cha “Ngoswe; Penzi Kitovu cha Uzembe” kuwakumbusha walimu wanaokwenda kuwafundisha makarani wa sensa kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

Sendiga alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria makarani ambao, kwa makusudi wataamua kuharibu kazi hiyo.

Alisema ulevi na uzembe ni kati ya vitu vinavyoweza kuharibu shughuli hiyo, ikiwa makarani hawatakuwa makini katika kutekeleza wajibu wao.

“Sio unachukua kishikwambi unakwenda baa au klabuni kwa sababu ya vijisenti ulivyopewa basi unakunywa mpaka unasahau kazi yako. Ole wako!” alisema.

Pia, aliwakumbusha makarani hao kuzingatia uvaaji, akisema suala la unadhifu halina mjadala, kwani muonekano wa karani huongeza imani kwa wanakaya atakaokwenda kuwahoji.

“Kina kaka mnyoe, pigeni scrub mpendeze, kina dada kuweni nadhifu. Nataka kuona mkoa wa Iringa tunafanya vizuri,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Dk Abeli Nyamhanga aliwataka walimu kutokunja sura kama wanakunywa sumu wakati wanapokwenda kufundisha makarani wa sensa.

“Ukifundisha huku umejiachia kwa upendo na tabasamu basi wanafunzi wako watafurahia somo lako, msifundishe kama mnakunywa sumu,” alisisitiza.

Chanzo Mwananchi

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments