Wachoma jengo la Bunge,Raia waandamana Libya

Waandamanaji wamevamia jengo la Bunge lililopo katika mji wa Tobruk kupinga kuzorota kwa hali ya maisha na mkwamo wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo, miaka 12 tangu kuuawa kwa Rais wao wa muda mrefu, Muammar Gaddafi.

Uvamizi huo ulitokea juzi kwa baadhi ya waandamanaji hao kuingia bungeni na kufanya uharibifu huku viongozi wakilikemea tukio hilo na wengine kuchoma matairi nje ya jengo hilo.

Hata hivyo, jengo hilo la Bunge lilikuwa tupu siku hiyo, kwani ni mwanzo wa mapumziko ya wikendi nchini Libya.

Bunge la Libya limehamishia makao makuu yake mjini Tobruk, kilomita 600 mashariki mwa Tripoli tangu mfarakano wa mwaka 2014 kufuatia uasi uliomwondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Muammar Gaddafi.

Serikali pinzani inayojulikana kama Baraza Kuu la Taifa, iko Tripoli. Picha zilizosambaa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zilionyesha mwandamanaji aliyekuwa akiendesha tingatinga akipenya sehemu ya lango na kuwaruhusu waandamanaji wengine kuingia kwa urahisi huku magari ya viongozi yakichomwa moto.

Baadaye, waandamanaji walianza kuvunja kuta za jengo hilo kwa vifaa vya ujenzi.

Wengine, waliokuwa wakipeperusha bendera za kijani za utawala wa Gaddafi aliyeuawa Oktoba 2011, walirusha nyaraka za ofisi hewani. Huku likitambua haki ya raia kuandamana kwa amani, Bunge lililaani uharibifu na uchomaji moto wa makao yake makuu.

Waziri Mkuu katika Serikali ya mpito yenye makao yake makuu mjini Tripoli, Abdulhamid Dbeibah aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba utafanyika uchaguzi.

Maandamano hayo ya wananchi yamefanyika zikiwa zimepita siku kadhaa kwa wananchi nchini Libya kushuhudia umeme ukikatika kutokana na kufungwa kwa vituo vya mafuta kulikochangiwa na migogoro ya kisiasa inayoendelea.

“Tunataka taa ziwake,” waandamanaji hao walisema.

Serikali mbili zimekuwa zikigombea madaraka kwa miezi kadhaa, moja ikiwa na makao yake mjini Tripoli ikiongozwa na Dbeibah na nyingine inayoongozwa na waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Fathi Bashagha aliyeteuliwa na Bunge na kuungwa mkono na mwanajeshi mwenye makao yake mashariki mwa nchi, Khalifa Haftar.

“Natoa wito kwa wabunge wenzangu pamoja na wajumbe wa Baraza Kuu la Serikali kujiuzulu kwa pamoja ili kuheshimu matakwa ya watu wa Libya na kulinda utulivu wa Libya,” mbunge Ziad Dgheim alinukuliwa na idhaa ya Libya Al-Ahrar Ijumaa iliyopita.

Mbunge Balkheir Alshaab alisema: “Lazima tutambue kushindwa kwetu na kujiondoa mara moja kwenye ulingo wa siasa.”

Uchaguzi wa Rais na wabunge uliopangwa kufanyika Desemba mwaka jana ulikusudiwa kuhitimisha mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa kufuatia kumalizika kwa duru ya mwisho ya ghasia ya mwaka 2020 lakini haukufanyika kwa sababu ya wagombea kadhaa wenye utata na kutokubaliana kwa misingi ya kisheria ya uchaguzi.

Alhamisi iliyopita Umoja wa Mataifa ulisema mazungumzo kati ya taasisi hasimu za Libya yenye lengo la kuondoa mkwamo uliopo, yameshindwa kutatua tofauti zao.

Spika wa Bunge, Aguila Saleh na Rais wa Baraza Kuu la Taifa, Khaled al-Mishri walikutana katika mazungumzo yaliyoitishwa na Umoja wa Mataifa (UN) jijini Geneva, Uswisi kwa siku tatu kujadili rasimu ya katiba ya uchaguzi.

“Ingawa baadhi ya mafanikio yalipatikana, hayakusaidia kusonga mbele kuelekea uchaguzi mkuu, huku pande hizo mbili zikiwa hazielewani kuhusu nani anaweza kugombea urais,” alisema mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams ambaye aliyewezesha mazungumzo hayo.

Matarajio ya uchaguzi yanaonekana kuwa mbali na tangu Bashagha alipoteuliwa, amekuwa akisisitiza kwamba muda wa Dbeibah umekwisha.

Baada ya Bashagha kushindwa kuingia Tripoli katika msuguano wa silaha hapo Mei, utawala hasimu umechukua madaraka eneo la mashariki katika mji wa Sirte alikozaliwa Gaddafi.

Hivi karibuni mapigano ya mara kwa mara yameshuhudiwa kati ya makundi yenye silaha mjini Tripoli na kusababisha hofu ya kurejea kwa mzozo mkubwa.

Maandamano ya juzi yalifanyika katika miji kadhaa ya Libya ukiwamo Tripoli ambako waandamanaji walibeba picha za Dbeibah na Bashagha.

“Maandamano ya wananchi yamezuka kote nchini Libya kwa kukerwa na kuporomoka kwa ubora wa maisha, tabaka zima la kisiasa lililotengeneza tatizo na Umoja wa Mataifa ambao umeshindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi,” Tarek Megerisi, mchambuzi kutoka Baraza la Umoja wa Ulaya na uhusiano wa kimataifa aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.

Shirika la Taifa la Mafuta la Libya lilisema Jumatatu iliyopita kwamba kusimikwa kwa mitambo ya mafuta katika eneo la Sirte kunamaanisha kuwa linaweza kutangaza nguvu kubwa, hatua inayoliweka huru kutoka kwenye majukumu ya kimkataba kutokana na mambo nje ya uwezo wake.

Mapema Aprili zuio liliwekwa kwenye vituo viwili vikubwa vya usafirishaji na vikosi vya Haftar vinadhibiti vituo vikubwa vya mafuta. Kupungua kwa uzalishaji wa gesi kulichangia kukatika kwa umeme kwa muda mrefu, hali inayoweza kudumu kwa karibu saa 12 kwa siku.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments