Wamiliki Wa Seattle Sounders Kumuunga Mkono Rais Samia Suluhu Kuinua Sanaa, Michezo

Kampuni kubwa ya Kimtaifa ya Vulcan Inc. kupitia kampuni yake tanzu ya Vulcan Arts and Intertainment iliyoasisiwa na mmoja wa waanzilishi wenza wa kampuni ya Microsoft akiwa na Bill Gates, Allen Paul, imeeleza kuwa iko tayari kusaidiana na Serikali ya Tanzania kuinua sanaa na michezo nchini.
Kampuni ya Vulcan yenye makao makuu mjini Seattle, Marekani, tayari imewekeza mabilioni ya dola katika sekta za michezo na sanaa ikiwemo kumiliki timu ya mpira wa miguu inayofanya vyema katika Ligi Kuu ya Soka ya nchini Marekani (MSL), Seattle Sounders FC; klabu ya michezo ya Sea Hawks, klabu ya mpira wa kikapu ya Portland Trailblazers inayoshiriki NBA na viwanja kadhaa vya michezo mbalimbali zaidi ya 20 ikiwemo uwanja mkubwa wa Lumen Field wenye uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 70,000 unaomilikiwa na klabu ya Sounders (ambao pia umeteuliwa kutumika kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026).

Aidha, kampuni hiyo inamiliki vituo kadha vya Makumbusho ikiwemo Makumbusho Kubwa ya Sanaa na Historia ya Utamaduni wa Hip Hop.
Akizungumza mjini Seattle Jumatano Juni 29, 2022, wakati wa ziara ya wawakilishi wa Waziri wa Michezo wa Tanzania, Mhe Mohammed Mchengerwa, walioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Dkt. Emmanuel Ishengoma, Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko na Ubia wa kampuni hiyo Luke Grothkopp amesema kampuni hiyo ilitaka kuwekeza Tanzania tangu miaka 10 iliyopita lakini kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao ubia huo haukuendelea.

“Mwanzilishi wa kampuni hizi ambaye sasa ni marehemu Bw. Allen, alifika Tanzania na alikuwa mtu wa masuala ya sayansi na uhifadhi wa mazingira na alipenda kufanya kazi na Tanzania lakini haikuwezekana. Leo sisi tuko tayari kuyaendeleza mawazo yake hayo kwa kuingia ubia wa kusaidia michezo na sanaa nchini Tanzania,” alisema Bw. Luke.
Aidha, amempongeza Rais wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki filamu ya Royal Tour akisema ni filamu ambayo imeongeza chachu ya kuwajulisha Wamarekani na watu wengine duniani uzuri wa Tanzania katika utalii na uwekezaji.

“Nimeitazama ile filamu na nitaiangalia tena. Ni maudhui ya kimataifa kabisa. Sisi pia tuko tayari kushirikiana nanyi kuitangaza Tanzania kwa kutumia klabu zetu za michezo na viwanja vyetu vya michezo.”
Naye Dkt. Abbasi ameikaribisha kampuni hiyo kushirikiana na Tanzania kwani Tanzania ni nchi iliyosheheni vipaji vya michezo na sanaa za aina mbalimbali na kuwaahidi ushirikiano wa wadau wote muhimu nchini Tanzania.
Na Mwandishi Wetu, Seattle, USA

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments