Wanafunzi Waliongoza 10 Bora Wataja Siri ya Mafanikio


 Wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kitaifa, wa Shule ya Sekondari Wari Wilaya Hai mkoani Kilimanjaro, Philipo Ng'eleshi (PCB) amesema siri ya mafanikio ni  kuongeza bidii ya kusoma.

Shule hiyo  inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi  ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo imetoa wavulana wawili kumi bora kitaifa, masomo ya sayansi, Philipo Ng'eleshi (PCB)  alishika nafasi ya (9) huku na Kennedy Mcharo  akishika nafasi ya (10) PCM.

 Akizungumza kwa njia ya simu julai 6, 2022   Mcharo amesema kuwa mazingira ya shule  yalikuwa rafiki kwa wanafunzi kutokana na kuwa nje kidogo ya mji  na kwamba ipo  sehemu yenye utulivu wa hali ya juu.

"Kwanza mazingira yalikua rafiki, shule ipo nje ya mji, upo utulivu wa kutosha na pia hali ya hewa ni ya baridi  sana ambapo mwanafunzi anaweza kujisomea kwa muda mrefu. Pia nidhamu ambayo wanafunzi tulijengewa tulipofika shuleni ilitusaidia sana kwani ukifika shuleni huwezi kujua kama wapo wanafunzi kutokana na utulivu uliopo,” amesema.

Mwenyekiti wa  Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, Daud Mrindoko amesema nidhamu na ushirikiano baina ya viongozi,  walimu pamoja na wanafunzi  ndio mwarobaini uliotumika kuhakikisha ufaulu katika Shule ya Sekondari Wari unaongezeka kwa kiwango cha kitaifa.

Mrindoko amesema baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita  jana  Julai 05, 2022 mwaka huu ambapo  shule hiyo  imefanikiwa kupata wavulana wawili waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya sayansi.

Mrindoko amesema  tangu aingie  madarakani mwaka 2017 kama mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi, mikakati ya kufufua na kuboresha shule zilizopo chini ya jumuiya hiyo iliwekwa ambapo mpaka sasa mafanikio yanazidi kuonekana.

"Ili kupata mafanikio lazima kuwe na upendo, kuwapa wanafunzi imani kuwa inawezekana na kuwafanya waalimu wajitambue  kupitia usimamizi mzuri na kutatua changamoto  zinazo wakabili waalimu pamoja na wanafunzi," amesema Mrindoko.

Amesema jumuiya hiyo inatambua juhudi zinzofanywa na walimu katika shule hiyo ambapo  wamekuwa wakitoa motisha kwa walimu na  wanafunzi wanaofanya vizuri shuleni hapo.

"Mwaka 2021 tulifanikiwa,  mwanafunzi mmoja alifanya vizuri na akaingia kwenye orodha ya  wanafunzi 10 walioongoza masomo ya sayansi kitaifa, na mwaka huu tumefanikiwa ambapo wanafunzi wawili wamefanya vizuri kwenye masomo ya sayansi kitaifa, haya ni mafanikio makubwa,” amesema.

Mkuu wa shule hiyo, Naomi Kikoti amesema  kuwa  siri kubwa ni kufanya kazi kwa pamoja (team work) kati ya viongozi, walimu na wanafunzi  na kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka kwa kudhibiti  wanafunzi   kuwa na nidhamu  ya hali ya juu.

 " Walimu wetu wanajitahidi kufundisha hata masaa ya jioni ili kuhakikisha wanamaliza mtaala mapema ili kuwapa wanafunzi muda mrefu wa kufanya marudio na kuwapa mitihani mingi ya kuwapima kati ya kidato cha tano na cha sita na pamoja na mashindano na shule nyingine zinazofanya vizuri," amesema  Kikoti.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments