Recent-Post

Wananchi Chunya walia na gharama kubwa za matibabu

Baadhi ya wananchi wilayani Chunya wamelalamikia gharama za matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo, huku pia wakilalamikia kauli mbovu kutoka kwa wahudumu.

Wakizungumza katika ziara ya Mbunge wa Lupa Masache Kasaka aliyefanya ukaguzi katika hospitali hiyo leo Julai 21, wananchi hao wamesema bei ya kulaza mgonjwa kwa siku ya Sh10,000 ni kubwa mno.

Kufuatia malalamiko hayo, Kasaka amekemea tabia ya wahudumu wa afya, huku pia akiitaka hospitali hiyo kupitia upya gharama za matibabu.

Akikagua jengo la bohari ya dawa na jengo la wagonjwa dharula (OPD), Kasaka amemshauri mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya kuhakikisha anakaa na bodi ya hospitali hiyo ili kuhakikisha wanatatua baadhi ya changamoto wanazolalamikia wananchi ikiwemo bei ya kulaza wagonjwa.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mgaga mkuu wa Wilaya ya Chunya, Darison Andrew amesema atahakikisha anakaa na wahudumu wa hospitali hiyo na kuzungumza nao kuhusu maadili ya kazi ili kuondoa changamoto zilizopo.

Kuhusu gharama za matibabu, amesema atahakikisha anaitisha bodi ya usimamizi wa hospitali ya wilaya ili kupitia upya bei ya kulaza mgonjwa.

Chanzo Mwananchi

Post a Comment

0 Comments