WANANCHI WILAYANI IRAMBA MKOANI SINGIDA KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI WA ZIWA VICTORIA

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, amewahakikishia wakazi wa Kata za Mgongo na Shelui Wilayani Iramba mkoani Singida, kwamba wataondokana na changamoto ya uhaba wa maji hivi karibuni kupitia mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria.

Dk. Nchemba, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, ametoa ahadi hiyo wakati alipozungumza na wananchi wa kata hizo ili kusikiliza fursa na kero mbalimbali zinazowakabili.

Wakazi wa Kata ya Mgongo walimpokea Dk. Nchemba kwa mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwemo kutaka kuondolewa adha ya upungufu wa maji ya uhakika unaowakabili, kuboresha miundombinu ya sekta ya afya, elimu pamoja na miundombinu ya barabara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano hiyo, wakazi hao walimpongeza Dkt. Nchemba, kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi hao na kwamba baadhi ya changamoto zilizowasilishwa kwake ni kiu ya kutaka kuona wanafunzi wanapata hosteli, Kituo chao cha afya cha Mgongo kinaboreshwa.

Dkt. Nchemba aliwaondoa hofu wakazi hao kuhusu tatizo la maji na kuahidi kuwa ndani ya siku 7, wataalamu wanaotekeleza mradi wa Maji wa Ziwa Victoria watafika kwenye kata hizo ili kuanza kuweka miundombinu ya kupitisha maji kuelekezwa kwenye kata hizo za Mgongo na Shelui.

“Msiwe na mashaka maji ya Ziwa Victoria yatafika Mgongo na Shelui, ninachowaomba wananchi ni kutoa ushirikiano kwa wataalam hao wanaotekeleza mradi ili muwaoneshe jiografia ya maeneo ambayo watapitisha miundombinu ya maji” Alisisitiza Dkt. Nchemba.

Kuhusu barabara, miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa na hosteli, Dkt. Nchemba aliwataka wananchi hao kusubiri kukamilika kwa ujenzi wa barabara unaendelea lakini pia aliahidi kutuma wataalam watakaofanya tathimini ya gharama za ukamilishaji wa Hosteli ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mgongo na kuanza ujenzi maramoja kwa kuwa fedha zipo.

Aidha, Dkt. Nchemba aliiagiza Bodi ya Maji ya Kata ya Mgongo, kuitisha mkutano na kuwasomea wananchi mapato na matumizi ya fedha za mradi wa maji wa Kata hiyo baada ya wananchi kulalamika kuwa Bodi hiyo haijawasomea mapato na matumizi kwa kipindi cha miaka 2 na kwamba Bodi hiyo inafanya matumizi bila kuwepo vikao.

“Kamilisheni jengo kwa ajili ya kufunga jenereta ili wananchi wapate maji ndani ya siku tatu na mkikamilisha itisheni mkutano muwaeleze wananchi fedha zao zimetumikaje, huo ndio utawala bora” alisema Dkt. Nchemba.

Akiwa katika eneo la Nselembwe, Kata ya Shelui, Dkt. Nchemba aliwasihi watanzania wamwombee Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, afya njema ili aweze kutimiza dhamira yake njema ya kuwaletea wananchi waendeleo ya haraka.

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ikiwemo uamuzi wa kuifanya elimu kutolewa bure kuanzia shule za awali hadi kidato cha sita, na kuelekeza rasilimali kubwa ya fedha katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha kwenye shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, uvuvi na kuendeleza wajasiriamali.

Akiwa Wilayani Iramba, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alikagua ujenzi wa barabara ya Shelui hadi Nkyala na barabara ya Tindigulu hadi Kidalu na kuelezea kufurahishwa kweke na maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Iramba.

Wakazi wa Kata ya Mgongo, wilayani Iramba mkoani Singida, wakiwa wamembeba Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alipowasili katika eneo la Mgongo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.


Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akisalimiana na wananchi wa Kata ya Shelui, Wilayani Iramba, mkoani Singida wakati alipofanya mkutano na wananchi wa kata hiyo.
Chanzo CCM Blog Taifa

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments