Recent-Post

Wauguzi Kuweni Marafiki Wazuri Wa Ndugu Wa Wagonjwa Mnaowahudumia

Wauguzi wanaotoa huduma kwa wagonjwa wa dharula na mahututi wametaki kuwa marafiki wazuri wa ndugu wa wagonjwa wanaowahudumia kwa kutoa taarifa sahihi za maendeleo ya mgonjwa kwa kufanya hivyo kutapunguza malalamiko yasiyo ya lazima.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo wakati akifunga mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini.

Dkt. Delilah ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi alisema baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakiona kama ndugu wa wagonjwa ni wasumbufu lakini hakuna ndugu msumbufu kwani anahitaji kujua maendeleo ya mgonjwa wake.

“Katika kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi kuna uhusiano wa karibu kati ya mgonjwa, mtoa huduma na ndugu wa mgonjwa wote hawa watatu kuna hali ambayo wanaipata wakati wa kuuguza. Toeni taarifa ya kila siku ya maendeleo ya mgonjwa kwa ndugu zake na kuwaambia ukweli kila hatua anayopitia”,.

“Wagonjwa wengi walioko katika Uangalizi Maalum ICU hawawezi kula zaidi ya kutumia dawa utakuta ndugu wa mgonjwa anakwenda na chupa iliyojaa uji akija jioni anaikuta chupa imejaa anabaki kujiuliza mbona hajala na ikitokea mgonjwa huyo kapoteza maisha ataamini amekufa kwa njaa kitu ambacho siyo kweli na inakuwa hivyo kwasababu hamtoi taarifa kwa ndugu. Kutoa taarifa katika hali ya upole ili wawaelewe ni sehemu ya maadili yenu ya kazi kwa kufanya hivyo mtapunguza malalamiko”, alisema Dkt. Delilah.

Kuhusu kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi Dkt. Delila alisema kama saikolojia ya mtoa huduma haiko vizuri asiihamishie kwa mgonjwa na siyo vizuri kufanya hivyo kwani anamtegemea inaweza kuwa anatambua au hatambui kwani hata wasiokuwa na fahamu wanaelewa kile kinachoendelea.

“Mpe mgonjwa taarifa ya kile unachotaka kukifanya kwake hata kama hajitambui fahamu kuwa anaelewa kila kinachoendelea hivyo basi kama vile unavyofanya kwa mgonjwa ambaye anaelewa fanya hivyohivyo na kwa yule ambaye hakuelewi iwe anasikia au la wewe fanya tu”,alisema Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo.

Aidha Dkt. Delila aliwapongeza wauguzi hao kwa kutenga muda wao na kwenda kujifunza kozi hiyo na kuwasihi wasiache kusoma na watumie simu zao za viganjani kusoma masomo ya mtandaoni ya critical care nurses kwani kama wataacha kusoma watasahau yale waliyojifunza.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt.Peter Kisenge alisema kozi hiyo ilianza Januari mwaka huu imemalizika salama na wanafunzi wamefaulu vizuri anaamini kwa jinsi walivyofaulu wataenda kuitumia elimu hiyo kwa kuwasaidia na kuokoa maisha ya wagonjwa pia watawafundisha wenzao waliowaacha katika Hospitali walizotoka ili nao wapate elimu hiyo kwani wagonjwa wanaoumwa sana ambao wamelazwa ICU wanahitaji kuishi.

“Mkafanye mabadiliko makubwa katika Hospitali mlizotoka kwani wauguzi wanaotoa huduma za ICU kwa wagonjwa wa dharula na mahututi wanakitu maalum ndani yao cha kuwasaidia wagonjwa wenye hali ngumu ambao wanaweza kupoteza maisha yao wakati wowote lakini kupitia Mwenyezi Mungu wao wanaweza kuokoa maisha ya wagonjwa hao kitu ambacho watu wengine hawana”,.

“Ninaipongeza Serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuwasomesha wataalamu, kujenga majengo ya kisasa zikiwemo ICU na kununua vifaa tiba vya kisasa. Wafanyakazi hao wanafanya kazi katika ICU na ndiyo waliowafundisha nyinyi kwani bila kuwepo kwa wataalamu hao msingeweza kupata mafunzo”, alisema Dkt. Kisenge.

Naye mratibu wa kozi hiyo ambaye ni Afisa uuguzi na mtaalamu wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi Joshua Ogutu alisema washiriki wa kozi hiyo ambao walikuwa 13 wamejifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa aliyepo katika mashine ya kumsaidia kupumua (Ventilator)na jinsi ya kutumia mashine hiyo.

Jinsi ya kutumia mashine ya Cardiac Monitor ambayo inafanya uangalizi wa karibu kwa wagonjwa mahututi na kuushtua moyo ulioacha kufanya kazi (Defibrillation).

Pia walijifunza matumizi ya mashine inayosafisha damu ya mgonjwa wa figo na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa anayehitaji huduma ya dharula, jinsi ya kutoa tiba maalum za wagonjwa wa figo, kutoa dawa za wagonjwa wa moyo na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa ambaye moyo wake haufanyi kazi vizuri (Basic Life Support – BLS, Advanced Cardiac Life Support – ACLS).

Afisa Uuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando Archileus Dominick ambaye ni mshiriki wa kozi hiyo alisema mafunzo yalikuwa mazuri na wamejifunza vitu ambavyo walitarajia kujifunza na vingine ambavyo hawakutarajia kujifunza katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa mahututi na dharula na anaamini kozi hiyo itamsaidia kutoa huduma bora kwa wagonjwa hao kwani hapo awali alishindwa kuwahudumia ipasavyo kwakuwa hakuwa na ujuzi wa kutosha.

Epifania Mlay ambaye ni Afisa Uuguzi kutoka Hospitali ya Rabininsia iliyopo jijini Dar es Salaam aliyeshiriki kozi hiyo alisema jinsi alivyokuwa kabla hajahudhuria mafunzo hayo ni tofauti na alivyokuwa sasa kwani amefundishwa vitu vingi ambavyo hakuwa anavijua lakini alikuwa anaviona vikitokea Hospitalini aliwasihi wauguzi wenzake kuomba kozi hiyo pindi itakapotangazwa kwani itawaongezea uwezo binafsi wa kufanya kazi.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianzisha kozi hiyo ya wiki 27 ambayo inafanyika mara mbili kwa mwaka lengo likiwa ni kuhakikisha wauguzi ambao ndiyo wanakaa na wagonjwa muda mrefu wodini wanapata elimu ya kutosha ya jinsi ya kuwahudumia wagojwa wa dharula na mahututi ambayo itasaidia kupunguza vifo vinavyotokea ICU.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akifunga mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wauguzi 13 yamefungwa leo jijini Dar es Salaam.Mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) ambao ni wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini wakati wa ufungaji wa kozi hiyo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) ambao ni wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini wakati wa ufungaji wa kozi hiyo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akimkabidhi cheti Afisa Uuguzi Scola Riwa baada ya kuhitimu mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wauguzi 13 yamefungwa leo jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akimkabidhi cheti Afisa Uuguzi Hamisi Mang’oly baada ya kuhitimu mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wauguzi 13 yamefungwa leo jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa Maafisa Uuguzi 13 kutoka hospitali mbalimbali nchini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo na washiriki wa mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharula na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa Maafisa Uuguzi 13 kutoka hospitali mbalimbali nchini mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha na Khamisi Miharo

Post a Comment

0 Comments