Wizi Daraja la JPM Bado, RC Gabriel Atoa Maagizo

Ikiwa imepita miezi miwili tangu Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kutoa taarifa ya kuwakamata watu 10 kwa tuhuma za wizi wa vifaa katika daraja la JPM (Kigongo-Busisi), inaelezwa wizi wa vifaa hivyo bado unaendelea.

Kutokana na kuendelea kwa vitendo hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel ameliagiza Jeshi la Polisi mkoa huo kufanya doria saa 24 na msako kwenye magari na watu wanaopita katika eneo hilo ili kudhibiti uhalifu huo.

Pia, amemtaka Mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya CCECC kutoa boti kwa askari wa Jeshi la Polisi kufanya doria usiku na mchana ndani ya mita 300 kuzunguka linapojengwa daraja hilo katikati ya Ziwa Victoria ili kukomesha wanaochomoa vyuma na kuvitorosha kwa kutumia mitumbwi na boti.

"Kuna watumishi wengi ambao wapo hapa. Kwa mazingira hayo kuna changamoto ya usimamizi, kuna watumishi wachache ambao wanachukua vyuma katika eneo hili, kuanzia leo tunaongeza ulinzi wa hali ya juu katika eneo hili," amesema Gabriel

Awali akizungumza leo Julai 4,2022 wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mwanza, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose amesema ujenzi wa mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh602 bilioni umefikia asilimia 47.4 huku akisema unatarajiwa kukamilika itakapofika Februari 28,2024.

Pia ametaja changamoto katika utekelezaji wa mradi huo kuwa ni baadhi ya watu kufanya hujuma kwa kwa kutumia mitumbwi na magari binafsi kuiba vifaa ikiwemo vyuma chakavu vinavyotumika kwenye ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa kilomita 3.2.

"Tunatarajia mradi utakamilika kwa wakati japo kuna changamoto ya wizi kukithiri katika eneo hili. Tunaamini baada ya maagizo haya ya Mkuu wa Mkoa wizi huu utakomeshwa" amesema Ambrose

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Idetemya wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Edward Dawson ameahidi kuitisha kikao cha dharura katika eneo lake ili kuweka mikakati ya kuanzisha ulinzi shirikishi kukomesha vitendo hivyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments