DKT. NCHEMBA AFANYA ZIARA YA KUSHITUKIZA SOKO KUU LA KARIAKOO DAR ES SALAAM

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na Jumuiya ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam, baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi ikiwemo msuguano baina yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kuhusu masuala ya kodi na risiti za kieletroniki.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alieyevaa skafu ya Bendera ya Taifa-Meza Kuu) akisilikiza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alieyevaa skafu ya Bendera ya Taifa, akisilikiza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akisilikiza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushitukiza Sokoni hapo. Kulia ni Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Azan Zungu, na kushoto ni Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Herbert Kabyemela

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kwenye skafu ya rangi ya Bendera ya Taifa), akikatiza Mitaa ya Kariakoo alipofanya ziara ya kushitukiza kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Azan Zungu.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Dar es Salaam)

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiagiza mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo ili kuchochea biashara katika soko hilo linalotegemewa na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Dkt. Nchemba ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya ghafla katika Soko hilo akiambatana na Naibu Spika Na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azan Zungu, Mkuu wa Wiaya ya Ilala Bw. Ng’wilabuzu Ludigija na Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA

Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo walieleza changamoto zao mbalimbali zinazowakabili ikiwemo madai ya kushuka kwa biashara ya Nje kutokana na ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa wafanyabishara wa kigeni, ukaguzi ambao walidai si rafiki.

Walisema kuwa wafanyabiashara kutoka nje wanasumbuliwa kwa kudaiwa kuwa risiti wanazopewa na wafanyabiashara baada ya kununua bidhaa hazikuwa sahihi na kuzuiwa mizigo yao hali inayosababisha usumbufu kwa wageni na kumwomba Mheshimiwa Waziri Nchemba aingilie kati ili kufufua biashara katika Soko hilo.

Aidha, Wafanyabiashara hao waliiomba Serikali iongeze kiwango cha mfanyabiashara kusajiliwa kuwa mlipakodi wa VAT kutoka shilingi milioni 100 hadi shilingi milioni 500 ili kusisimua biashara zao na kuongeza mzunguko wa fedha utakaowasaidia kukua na kuwa wafanyabiashara wakubwa.

Ili kupunguza changamoto za kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali, wafanyabishara hao walipendekeza kodi zote ziwe zinatozwa bandarini wakati mizigo inapoingia nchini na kuacha biashara katika Soko la Kariakoo iendelee bila bughudha za masuala ya kodi.

Aidha, Wafanyabiashara hao waliwalalamikia baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wasio waaminifu wanaotumia mwanya wa makosa yanayofanywa na baadhi ya wafanybiashara kudai rushwa na kuikosesha Serikali mapato.

Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Mussa Azan Zungu alimwomba Mbeshimiwa Waziri Nchemba, kuwachukulia hatua kali watumishi hao wasiowaaminifu wanaotumia nafasi zao kujinufaisha kwa kudai na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara.

Aidha, Mhe. Zungu aliishauri Serikali ipunguze kiwango cha kodi ya mapato (VAT) ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi husika kwa urahisi na hiari zaidi hatua ambayo itakuza biashara na faida kwa wafanyabiashara nchini.

Akijibu hoja za wafanyabiashara hao waliokuwa wakimshangilia mara kwa mara, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, aliiagiza TRA kukutana na wafanyabiashara hao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Alisema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameelekeza mazingira ya kufanyiabiashara kwa wafanyabiashara nchini yaboreshwe ili kundi hilo liweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza ajira.

Aliahidi kuwa katika mwaka wa Fedha ujao wa 2023/2024 kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kikodi ikiwemo kupunguza VAT na kuja na utaraibu mzuri utakaohamasisha na kukuza biashara nchini.

Aidha, aliahidi kuwa Serikali itaongeza kiwango cha masharti ya wafanyabiashara wanaostahili kusajiliwa kwenye VAT kutoka kiwango cha sasa cha na VAT cha shilingi milioni 100 na kuwekwa kiwango kipya mwaka mpya wa bajeti utakapofika kwa sababu kiwango hicho cha sasa ni cha chini ikilinganishwa na ukubwa wa biashara zinazofanyika.

Dkt. Nchemba aliiagiza pia TRA kutozuia mizigo ya wafanyabiashara wa kigeni wanaonunua bidhaa zao katika Soko la Kariakoo na kuwataka washughulike na wafanyabiashara wasiowaaminifu waliotenda makosa husika kwa kuwa mifumo ya ndani ya nchi haiwahusu wafanyabiashara hao.

Katika hatua nyingine, aliwataka wafanyabiashara hao kuwa waaminifu na kufanyabiashara kwa kufuata misingi mizuri iliyowekwa ikiwemo kutoa risiti halalali zinazolingana na bidhaa walizouza ili kuepuka usumbufu.

Aidha, Dkt. Nchemba aliwaonya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wasiowaaminifu wanaojihusisha na vitendo vya kudai na kupokea rushwa na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na kuwataka wafanyabiashara hao kutoa taarifa ya watumishi wa namna hiyo wanaoikosesha Serikali mapato.

Kwa upande wake Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, aliyemwakilisha Kamishna Mkuu katika ziara hiyo ya kushtukiza, Bw. Herbert Kabyemela, aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na wafanyabiashara hao na kubainisha kuwa tatizo kubwa linaloikabili Mamlaka hiyo ni suala la ukosefu wa uaminifu wa wafanyabiashara hususan katika kutoa risiti zinazolingana na bidhaa wanazouza.

Dkt. Nchemba aliwaahidi wafanyabiashara hao kwamba atarejea tena sokoni hapo hivi karibuni kusikiliza kero na changamoto zao na kwamba mkutano huo alioufanya utaleta mabadiliko ili Soko hilo la Kariakoo liendelee kuchangia mapato ya Serikali na uchumi wa wafanyabiashara kwa ujumla

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments