SHAKA ATAKA WASOMI WATAMBULIWE NA KUWEZESHWA ILI WAWEZE KUJIAJIRI KAMA NJIA KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA

 Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ametaka wasomi watambuliwe kisha wawezeshwe ili kufikia hatma ya kujiari kama njia mojawapo ya kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.


Shaka amesema hayo leo alipotembelea Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro, ambapo amepata fursa ya kuona katika mabanda huduma na teknolojia mbalimbali kuhusu kilimo na ufugaji na kusema kwenye maonesho hayo liko jambo la faraja ambalo ameliona.

“Kupitia maonesho haya mimi kwangu naona ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anaelekea kufanikiwa kwa namna ambavyo vijana wameshawishika na kuamua kuwekeza katika sekta hii ya kilimo.

Tumewatembelea vijana wadogo ambao wote na kila mmoja ameweza kutafsiri maono ya Rais kwa aidha kwa kufikiria kuanzisha kitengo cha kuwasaidia vijana wenzake au kuwekeza kwenye masuala haya ya kilimo", amesema Shaka na kuongeza;

“Taasisi za kifedha wameonesha utayari wao wa kusaidia sekta ya kilimo, sasa pamoja na kwamba Rais ametenga bajeti kubwa kwa ajili ya sekta hiyo kwenye hili mimi natoa mwito kwa Wizara ya Kilimo na Serikali, kuweka mipango mizuri na madhubuti ili fedha hizi zinazotengwa na taasisi hizo za kifedha nazo ziweze kuyanufaisha makundi ambayo nimeyasema.

Kwa mkoa huu wa Morogoro uko mfano mzuri sana tunacho Chuo cha Kilimo Morogor, nadhani tukiwekeza pale yatapatikana matokeo chanya, kwani kila mwaka vijana wanahitimu , tukiwa na takwimu sahihi za vijana wangapi wanaohitimu na kutambua maeneo wanayotoka kisha Serikali ikatenga maeneo maalum kila kijana ikampa wastani wa heka japo tano na mashirika ya fedha nayo yakatoa fedha kwa vijana hao naamini changamoto ya ajira iliyopo kwa vijana inaweza kupungua kwa kiasi kikubwa".

“Hilo linawezekana na tujifunze nchini Misri ambao wenzetu wameweza kwa njiia kama hiyo na sisi Tanzania tunaweza zaidi ya hapo lakini lazima kuwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha vijana hawa tunawaandaa tangia wanamaliza au wanahitimu vyuo vikuu hadi wanaingia kwenye soko la ajira,”alisema.

Shaka alisema kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu ameiona dhamira ya Serikali kuuhuisha na kuunganisha vijana kutumia sekta ya kilimo kama mkombozi katika kujenga uchumi.

Aidha alisema lingine ambalo analiona kwenye suala la kilimo lazima waambizane na wawe tayari lakisi sio kuwa tayari tu wakati umefika sasa Watanzania kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuweza kufanya kilimo chetu vizuri.

Katika hatua nyingine Shaka alisema kwenye maonesho ya mwaka huu ameshudia mabadiliko na maboresho makubwa na yote yanaonesha utayari wa viongozi katika kutafsiri dhana na dhima waliyonayo kwa vitendo ya kusimamia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa mwaka huu yapo mambo kadhaa tumejifunza nadhani tunafahamu kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu lakini tunafahamu kilimo tunakitegemea kwa asilimia 70 ndani ya nchi yetu katika kuendesha maisha yetu ya kila siku lakini pia kunyanyua uchumi wa nchi yetu.

“Sasa kwa mwaka huu tunaongozwa na dhamira ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko katika sekta hii ya kilimo, wote tumeshuhudia ukitaka kutafsiri na kujua namna gani ambavyo Rais anaitazama sekta ya kilimo kama mkombozi kwa watanzania namna ambavyo ameweza kufanya mabadiliko makubwa,”alisema.

Aliongeza hata baada ya uhuru wa nchi hii haijapata kutokea bajeti ya mwaka 2022/2023 Rais Samia ametenga fedha karibia Sh.bilioni 954 ukingalisha na bajeti ya mwaka 2021/2022 ya Sh.bilioni 254 karibia asilimia 224 ya ongezeko hilo la bajeti.

“Lengo kuonesha mkazo zaidi katika Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza nguvu huko na dhamira kubwa ikiwa kuwaomboa vijana pamoja na wanawake.

“Katika hilo Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imeahidi katika kipindi cha miaka mitano tutazalisha ajira milioni nane kwa watanzania , sasa kwenye kutafsiri maelekezo ya Ilani Serikali ya Rais imeshajiwekea muekelekeo ama imeshajiwekea matatarajio yake katika ajira hizo,”alisema Shaka.

Alifafanua Serikali inatarajia mpaka kufikia 2025 karibia ajira milioni tatu zitakuwa zimezalishwa kupitia sekta hii ya kilimo huku akiongeza hayo ni mageuzi makubwa na huo ni ukombozi kwa vijana na wanawake.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akitazama ndege isiyo na rubani (drone) katika banda la Bodi ya Sukari katika maonyesho ya kilimo (Nanenane) mkoani Morogoro. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akiwa katika baadhi ya mabanda yanayoshiriki maonyesho ya kilimo (Nanenane) mkoani Morogoro. (PICHA NA CCM MAKAO MAKUU

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments