CCM KUFUATILIA UTENDAJI KAZI WATEULE WA RAIS

Katibu  wa Halmashauri Kuu ya Taita (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama kinafuatilia kwa karibu mienendo ya wateule wote wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuona kama wanatekeleza wajibu wao wa kumsaidia katika kuwatumikia Watanzania.


Shaka ametoa kauli hiyo Septemba 8,2022 alipozungumza na waandishi wa vyombo vya habari nchini kutoa taarifa ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika juzi, chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“CCM inawajibu wa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wetu na kupitia hadhara hii niowambe na kuwasihi wasaidizi wa Rais washuke chini kwa wananchi kwenda kusikiliza changamoto, kuwasikiliza wananchi.

“Tumetoka ziara juzi katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza, ni kweli ziko changamoto kadhaa ambazo sio lazima Rais ashuke kwenda kutatua lakini wasaidizi wakijipanga vizuri changamoto hizo zinaweza kutatuliwa, kwa hiyo niwaombe na niwasihi sana wote waliopewa dhamana na Rais Samia.

“Nia ya Rais ni njema sana na bahati nzuri Rais Samia amekuwa wa mfano na aliyotupa dhamana karibia wote ni vijana, tena vijana wadogo ambao damu inachemka. Nadhani tunacho kitu cha kulipa kwa Rais Samia na kitu cha kulipa pekee ni kujituma kwa bidii,” amesema.

Shaka ameongeza kitu pekee cha kulipa kwa Rais ni kutimiza majukumu yao na kuonesha uzalendo wao na vijana ambao wamepewa dhamana na Rais ni vema wakajituma.

“Tukionesha uzalendo wetu tunakwenda kuwawakilisha vizuri vijana wenzetu na tutampa moyo pia kuendelea kuwaamini vijana wengine wapate nafasi kwani Rais wetu hatizami huyu anatoka wapi, anatoka chama gani.

“Yeye akiona huyu anaweza kumsaidia anampa dhamana, kwa hiyo tunaombea vijana wengine wapate fupa na kwenda kuonesha uwezo wao. Tutaendelea kuwakumbusha ni wajibu wetu na kama Chama kuwakumbusha na kuwasihi wasadizi wa Rais washuke chini kwenda kutatua changamoto na kero za wananchi wetu tunaowangoza na kwenye hili niwaambie kwenye Chama tumekuwa wakali sana,” amesema Shaka.

Ameongeza Chama kinafuatilia kwa karibu mienendo ya wateule wote kwani ndicho kilichopewa dhamana huku akitoa mfano kuwa katika utoaji huduma kwa wananchi ni sawa sawa na kumiliki mali ambapo kuna tajiri, muuzaji na mnunuzi.

“CCM ni tajiri na Serikali ndio wauza duka lakini wateja wao ni wananchi, hivyo lazima yatengenezwe mazingira rafiki ya kuuza bishara yao na ikiuzwa vizuri kazi yao ni ndogo 2020/2025, sababu tumetoka huko (mikoani) tumeona walio wengi bado wana imani na Chama Cha Mapinduzi.

“Walio wengi bado wanaona CCM ni tumaini lao, kwa hiyo ikiuzwa vizuri biashara yetu mapato yake, manufaa yake na faida yake itakuwa kubwa 2020/2025. Kwa hiyo niseme kwa ufupi tu tunafuatilia kwa karibu mienendo na uwajibikaji wa wateule wote waliopewa dhamana na Rais,” amefafanua.

Amesema dhamira ni kuona kama wanatimiza lengo ambalo Rais Samia anatamani kuona wakilitekeleza wakati anawapa dhamana hizo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments