Diwani Agawa BIMA Ya Afya Ya ICHF Kwa Wanafunzi Wote Waliofanya Vizuri

 Na John Walter-BabatiKatika kutoa hamasa kwa wanafunzi wa darasa la Saba kufanya vyema katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya Msingi, Diwani wa kata ya Nangara, mjini Babati mkoani Manyara ametoa kadi za Bima za Afya (Ichf) kwa wanafunzi katika kata hiyo.


Akikabidhi bima hizo Diwani wa kata ya Nangara John Samweli Baran amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwapa morali ya kujifunza kwa bidii na kwamba atakuwa akifanya hivyo kila mwaka kwa wanafunzi watakaokuwa wanafanya vizuri kwenye mitihani yao kwenye shule zote tatu za msingi na moja ya Sekondari.

Amesema bima hizo zitawasaidia watoto hao kupata matibabu pindi wanapougua na kuwapunguzia wazazi au walezi gharama za kutibia ikiwa ni moja kati ya ahadi aliyoitoa wakati akiomba nafasi ya udiwani katika kata hiyo.

Afisa kutoka ofisi za Bima (Ichf) Halmashauri ya mji wa Babati Elibariki Michael amesema bima walizopewa zitawasaidia watoto hao kutibiwa kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa popote watakapokuwa na kadi zao.

Mkuu wa shule ya Msingi Ziwani Samwel Mrita amesema tukio hilo alilolifanya Diwani Samwel Baran ni muwashowasho kwa wanafunzi na kwamba itawafanya wafanye vizuri Kitaaluma, michezo, usafi wao na mazingira.

Nao baadhi ya Wazazi wamempongeza Diwani wa kata ya Nangara Samwel Baran kwa kutoa msaada huo wa bima huku wakiahidi kusisitiza watoto wao kujiibidisha katika masomo yao.

Aidha Wanafunzi wa shule ya msingi Ziwani, waliopewa Bima hizo na vifaa vingine wamemuahidi diwani huyo kufanya vizuri katika mtihani wa mwisho wa darasa la saba unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.




TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments