KAMATI KUU YA CCM YATOA AZIMIO KUMPONGEZA RAIS SAMIA, DK.MWINYI

 KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuiongoza ya Serikali na kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi


Akizungumza leo Septemba 8,2022 wakati akitoa taarifa ya kikao cha Kamati Kuu ,Katibu wa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kimepokea na kujadili taarifa kutoka vitengo vya Chama.

Amefafanua Kamati Kuu ilijadili kuhusu utekelezaji wa kazi za CCM na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo baada ya kujadili kwa kina ilifikia maamuzi kadhaa.

Shaka ameyataja maamuzi hayo ni kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoendelea kuiongoza Serikali na kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika kuimarisha huduma za kijamii, ustawi wa wananchi, kukuza uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja ili kuharakisha maendeleo endelevu.

Ameongeza miongoni mwa maeneo muhimu yaliyopewa kipaumbele ni sekta ya kilimo kupitia Bajeti ya Serikali ya 2022/2023, imeweka msukumo mkubwa katika kuboresha kilimo kwa kutenga sh. bilioni 954 likiwa ongezeko la asilimia 224.

“Fedha katika bajeti hii zimeelekezwa katika ruzuku ya mbolea kwa ajili ya kuongeza tija na kushusha bei ya pembejeo kwa wakulima pamoja na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

“Serikali imetambua kilimo cha kisasa kitaongeza ajira, kipato cha wakulima, kitaiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuimarisha uzalishaji na uchumi wa nchi,” amesema Shaka akitoa taarifa ya Kamati Kuu.

Pia amesema Kamati Kuu imempongeza Rais Samia kwa namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayoiongoza ilivyotekeleza na kusimamia mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania imeitekeleza kidijitali.

Amesema Sensa ni msingi muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango na program mbalimbali za maendeleo inavyowagusa wananchi moja kwa moja huku akieleza Kamati Kuu ya CCM pia imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi.

“Kamati Kuu imempongeza Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa jinsi ambavyo ameendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kiuchumi na kijamii kwa mafanikio makubwa pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi na ufisadi ambavyo vinarudisha nyuma na kudumaza jitihada za maendeleo,”amesema Shaka.

Katika hatua nyingine Shaka amesema mchakato wa kuwapata wagombea Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ambapo Chama kinaendelea na utaratibu wa ndani, ambapo ukikamilika Chama kitatoa taarifa.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments