Kingereza cha wabunge kinavyoakisi mianya ya elimu nchini

Mjadala ulioibuka katika mitandao ya kijamii kutokana na changamoto za umahiri wa kujieleza kwa Kiingereza, kwa baadhi ya wabunge na wagombea ubunge wa Afrika Mashariki, unahusishwa na kasoro za mfumo wa elimu kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine, ni kiashiria kwamba Tanzania haijajipanga na kuwekeza vilivyo ili kuitumia lugha hiyo katika shughuli na nyanja mbalimbali.

Kuibuka kwa mjadala huo kulitokana na kile kilichoshuhudiwa wakati wa kampeni za wagombea wa ubunge wa Afrika Mashariki (EALA), ambao kulingana na kanuni za Bunge, walitakiwa kutumia Kiingereza kama lugha ya kujieleza na kuombea kura.

Katika mchakato huo, mbali ya Kiingereza kuonekana kuwashinda wengi, kulidhihirika pia udhaifu katika maeneo kama vile ujenzi wa hoja, umakini wa kusikiliza maswali, kutojiamini na ukosefu wa stadi za kuzungumza mbele ya hadhara; haya yote yanatajwa kuwa na uhusiano na mchakato wa utoaji wa elimu nchini.

Ni kwa sababu hiyo ambayo baadhi ya wachangiaji kwenye mijadala hawakusita kusema kuwa ilikuwa ni aibu ya kujitakia kwa kukikumbatia Kiingereza, kuliibuka vimbwanga kadhaa vilivyosababisha kicheko sio kwa waliokuwa bungeni, hata kwa waliokuwa wakifuatilia matangazo yake.

Miongoni mwa wabunge hao waliozua vicheko ni Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’ wa Geita Vijijini ambaye mbali na kigugumizi wakati wa swali lake, hata kuyapanga vema maneno ilikuwa changamoto, achilia mbali usahihi wa sarufi.

Alipopewa nafasi ya kuuliza swali, Musukuma ambaye hivi karibuni alitunukiwa shahada ya udaktari ambayo hata hivyo watu wengi wamekuwa wakiihoji, alianza hivi...“Thank you madam Speaker for give me this chance , Mr Mnyaa I want to ask you one question (Nataka kuuliza swali moja).

“Where are you (Uko wapi? aliuliza na kisha kusita)... What... did you do for last five years? (Ulifanya nini kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita),”

Musukuma ambaye kwa kawaida ana sifa ya kujiamini anapotetea hoja zake, aliuliza swali hilo kwa kurudiarudia, hatua iliyoibua vicheko kutoka kwa wabunge wenzake.

Si Musukuma pekee, changamoto katika lugha hiyo ilionekana pia katika swali la mbunge wa Lulindi, Ally Mchungahela kwa mgombea Thomas Malima.

Aliuliza.. ‘‘Thank you Mr. Honorable Speaker (Asante Bwana Spika), This region has been one among the dumping place of the foreign market, what is your strategy to alleviate the problem o dumping in this region of East Africa Community

Licha ya makosa kadhaa ya kisarufi, swali lake linaweza kutafsirika hivi...’’ “Kanda hii ni miongoni mwa dampo la soko la nje. Una mkakati gani wa kupunguza tatizo la utupaji taka katika eneo hili la Jumuiya ya Afrika Mashariki?”

Alitakiwa arudie swali, lakini Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, aliingilia kati na kulifuta swali hilo.


Mianya kwenye mfumo wa elimu

Kasoro hii ya umahiri wa kuizungumza lugha hiyo, uwezo mdogo wa kujieleza mbele ya umma, kushindwa kujenga hoja na kutojiamini, yametajwa kuwa mambo yanayoakisi kuwapo kwa tatizo katika mfumo wa elimu nchini, kama inavyoelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa shirika la HakiElimu, Geofrey Bonaventure.

Anasema mfumo wa elimu unasababisha wasomi kukosa maarifa, kwa kuwa wanafundishwa kwa lugha wasiyoielewa.

“Ndiyo maana tunasisitiza sana, ili kujenga maarifa lazima utumie lugha unayoielewa kwa ufasaha kuzungumza na kusikiliza,” anasema.

Changamoto za kukosa elimu kunakotokana na kikwazo cha lugha, anasema zinamsababisha mtu ashindwe kujipambanua na kuzungumza vema mbele ya wengi kwa kuwa anakuwa na ufinyu wa maarifa.

“Ili uzungumze lazima uwe na maarifa, lakini uwe na uwezo wa kupanga mawazo yako vizuri mwishowe uzungumze kitu chenye mantiki, ndiyo maana sisi (HakiElimu) tunataka lugha ya kufundishia na kujifunzia iwe Kiswahili.

“Halafu Kiingereza kifundishwe vizuri kwa ufasaha na walimu wazuri, yule mtu atakuwa na maarifa kichwani na hivyo kuyahamisha kwa lugha nyingine inakuwa rahisi,” anasema.

Hata hivyo, anasema hoja muhimu ni kushinikiza matumizi ya Kiswahili katika Bunge hilo.

Hoja hiyo inapigiwa msumari na msomi wa lugha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomas anayechambua kilichotokea kwa kusema:

“Kwanza tunahitaji mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki aweze kujieleza vizuri kwa Kiingereza kwa sababu inaonekana hadi sasa lugha inayotumika kwenye mijadala ya Bunge la Afrika Mashariki ni Kiingereza,” anasema.

Ili wawakilishi hao watumikie vema nafasi zao, anasema wanapaswa kuifahamu vema lugha rasmi inayotumika katika bunge husika.

“Hatuwezi kupuuzia umuhimu wa wao kuwa na uwezo wa kuchambua mambo na kuchangia kwenye mijadala kwa maslahi ya Taifa letu,” anasema.

Kilichotokea kutoka kwa baadhi ya wabunge kushindwa kukizungumza vema Kiingereza, anasema ni kielelezo cha ombwe la ufundishaji mahiri wa lugha hiyo.

“Kumbe kutojua Kiingereza siyo tatizo la miaka ya hivi karibuni. Mfumo wetu wa elimu ulianza kuwa na matatizo tangu zamani kwa sababu wale wagombea walioshindwa kujieleza vizuri kwa Kiingereza ni watu wazima ambao walisoma zamani,” anasema.

Anahofu changamoto hiyo huenda ikasababisha baadhi ya wawakilishi katika bunge hilo, kushindwa kuchangia chochote kwa kuwa lugha inayotumika ni Kiingereza.

“Hilo likifanyika hatutalazimika kuwahoji wagombea bungeni kwa Kiingereza. Wangeweza kuulizwa kwa Kiswahili na kupima uwezo wao wa kujenga hoja badala ya kujikita kwenye kujua Kiingereza pekee,” anasema.

Yote yaliyotokea, anabainisha kuwa ni kielelezo kwamba Kiingereza siyo lugha rafiki kwa Tanzania, unahitajika uwekezaji mkubwa katika kuifundisha.

“Tukuze zaidi matumizi ya Kiswahili na watu wawe huru kujieleza kwa Kiswahili na wakalimani watumike zaidi kuliko kuwaweka katika mazingira magumu ya kushindwa kuwasiliana,” anaeleza.


Kiingereza bado

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha St, John jijini Dodoma, Dk Shadidu Ndossa anasema kilichoshuhudiwa bungeni, kinadhihirisha kwamba Tanzania haina uwezo wa kukitumia Kiingereza kwenye shughuli nyingi kama inavyodhaniwa.

“Kwa hiyo lugha ya Kiingereza bado changa, uwezo wetu wa kuizungumza ni mchanga na Mungu ametujaalia tuna lugha nyingine ya kimataifa (Kiswahili) tuitumie kwa shughuli zetu za maendeleo, ustawi wa watu wetu na Kiingereza kitumike pale kwenye ulazima,” anasema.

Anasema mjadala huo wa kuwapata wabunge wa Afrika Mashariki ulijikita katika mambo mepesi, kutokana na lugha iliyotumika kutoeleweka vema.

“Waliokuwa wakiomba kura walivyojieleza na namna wabunge walivyouliza maswali na hata aina ya maswali yaliyoulizwa yalikuwa mepesi,” anasema.

Anatolea mfano Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ambaye licha ya elimu ndogo aliyonayo ya darasani, amekuwa machachari katika kujenga hoja na kuuliza maswali, lakini katika mchakato huo alikuwa kinyume chake.

Ingawa hoja ya msingi ni kuona wabunge gani wanaopatikana kusimamia maslahi ya Tanzania katika jumuiya hiyo, anasema lugha iliyotumika kujieleza imepoteza shabaha hiyo.

Kutokana na kilichojitokeza, Dk Ndossa anashangazwa na uamuzi wa kutumia Kiingereza katika mchakato huo, ilhali Kiswahili ndiyo lugha inayofahamika zaidi Afrika Mashariki.

“Ukienda Kenya wapo wanaozungumza Kiswahili, Rwanda Burundi na hata Congo, ninashangaa kwa nini bado kwenye baadhi ya taasisi zetu za Jumuiya ya Afrika Mashariki lugha ya Kiswahili inaonekana kama haifai, hili linasikitisha,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Ndossa, inashangaza mbunge anayewania nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki anashindwa kusimama kuwatetea Waswahili wenzake.

“Tunatarajia nani aje kusema Kiswahili ndiyo lugha inayopaswa kutumika, huwa tunaona marais wakikutana katika mikutano ya wakuu wa nchi, wanazungumza kwa Kiswahili, sasa sijui wakuu wa nchi wanazungumza Kiswahili lakini wabunge hawazungumzi hata kuomba kura inaonekana kama ni dhambi,” anasema.


Mfumo wa elimu tatizo

Bado mfumo wa elimu unatajwa kuwa tatizo na mratibu wa zamani wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Catherine Sekwao anasema, suala si kulazimisha kutumia Kiswahili, bali kuna shida kwenye mfumo mzima wa elimu uliopo nchini.

Anasema mfumo huo unafanya baadhi ya wahitimu wa shahada kutojua Kiingereza, ilhali ndiyo lugha iliyotumika kuwafundisha.

“Kama kuna wabunge wengine walioshindwa kujibu maswali kwa Kiingereza hiyo inadhihirisha kwamba kuna udhaifu katika ufundishaji wa Kiingereza,” anasema.

Hata hivyo, anafafanua udhaifu huo unasababishwa na kukosekana msimamo wa lugha rasmi ya kufundishia katika ngazi zote za elimu.

Iwapo kutakuwa na msimamo huo, Sekwao anasema uwekezaji utafanyika katika kufundisha lugha na hivyo wanafunzi wataielewa kwa kuiandika na kuizungumza.

Lakini, anasema sababu nyingine ya hali iliyotokea katika bunge hilo ni sifa za kisheria za mbunge nchini.

Anaeleza kulingana na utaratibu wa nchi, kigezo cha kuwa mbunge ni kujua kusoma na kuandika na aghalabu watu hao hawajui lugha tofauti na walizozaliwa nazo.

“Mtu kaishia darasa la pili amejua kusoma na kuandika, unatarajia aulize swali la Kiingereza? Kuna changamoto kwenye hili angalau vigezo vya kuwa mbunge vingebadilishwa kwa kuwa wanafanya kazi kubwa,” anasema.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments