Mkutano wa Mbatia wazuiwa, asema...

Mgogoro wa NCCR Mageuzi umeibuka kwa sura tofauti baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia kuzuiwa kufanya mkutano wake na waandishi wa habari.

Jana Jumamosi, mkutano mkuu wa dharura wa Kamati Kuu ya NCCR Mageuzi uliofanyika jijini Dodoma, uliazimia kumvua uenyekiti na uanachama Mbatia na wenzake.

Kuvuliwa kwake uanachama kulianza na kusimamishwa kufanya shughuli zote za chama hicho, uamuzi uliofanywa Mei 21, 2022 na Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi.

Katika hali ya kujibu uamuzi wa jana wa chama hicho, Mbatia aliitisha mkutano na waandishi wa Habari katika Hoteli ya Regency Park, Mikocheni jijini Dar es Salaam, leo Jumapili, Septemba 25,2022 kabla ya kuzuiwa kufanya hivyo.

Alipofika hotelini hapo saa 7:07 mchana, mmoja wa maofisa wa hoteli hiyo alimwambia amepokea maelekezo ya kusitisha mkutano huo, hivyo haruhusiwi kufanya tena.

Mbatia aliomba taarifa hiyo kwa maandishi na baada ya kupewa,hwaandishi wa habari walitakiwa kutopanda ghorofa ya nane, mahali palipopangwa kufanyika mkutano huo.

Badala yake, walitakiwa kuondoka eneo hilo, Mbatia aliposhuka chini kutoka ghorofani alitaka kufanya mkutano huo katika eneo hilo ambako pia alizuiliwa na ofisa huyo wa hoteli.

Baadaye, aliamua kufanya mkutano huo nje ya ukuta wa hoteli hiyo ambapo huko alifanikiwa.

Katika mazungumzo yake, Mbatia amesema anashangazwa na uamuzi wa kuzuiwa akidokeza kabla ya zuio hilo alishapigiwa simu na mamlaka kutakiwa ahirishe mkutano huo.

"Tumeambiwa kwamba wenye mamlaka za juu wamewaagiza (Regency Park Hotel) wasituruhusu kufanya mkutano hapa na mimi kabla sijafika hapa, nilipigiwa simu kwamba tuusitishe," amesema Mbatia.

Chanzo Mwananchi

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments