RPC SINGIDA: USHIRIKIANO UTASAIDIA KUTOKOMEZA BIASHARA HARAMU YA KUSAFIRISHA BINADAMU

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Relief Initiatives, Edwin Mugambila akizungumza katika semina ya siku nne iliyoanza leo Septemba 13 hadi Septemba 16 iliyowahusisha wasimamizi wa sheria mahakama, polisi, uhamiaji na ustawi wa jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo wa uelewa wa namna ya kushughulikia utokomezaji wa biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stellah Mutahibirwa akifungua semina hiyo.
Picha ya pamoja. Kutoka kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Relief Initiatives, Edwin Mugambila na ACP Ahmad Mwendadi kutoka sekretariat ya kitaifa ya kupambana na Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu nchini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stellah Mutabihirwa, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Allu Nzowa na SSI Felista Orden Sanga- Superintendent wa Uhamiaji Mkoa wa Singida,
Majadiliano wakati wa semina hiyo yakiendelea.

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stellah Mutahibirwa amesema mapambano ya kutokomeza biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu yatafanikiwa kwa ushirikiano baina ya Uhamiaji, Ustawi wa Jamii na jeshi la polisi idara ya dawati la jinsia.

Mutahibirwa ameyasema hayo leo wakati akifungua semina ya siku nne iliyoanza leo Septemba 13 hadi Septemba 16 iliyowahusisha wasimamizi wa sheria mahakama, polisi, uhamiaji na ustawi wa jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo wa uelewa wa namna ya kushughulikia utokomezaji wa biashara hiyo semina ambayo imeandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Relief Initiatives.

"Ushirikiano wa makundi haya ni muhimu sana ili kutokomeza biashara hii ambayo inakuwa kwa kasi na kuwahusisha watoto wenye umri kati ya miaka 12 hadi 15 na Mkoa wa Singida ukiwa ni miongoni mwa mikoa iliyoathiriwa na biashara hii" alisema Mutahibirwa

Mutahibirwa aliomba idara ya uhamiaji kujiridhisha ipasavyo utoaji wa hati za kusafiria zinazoombwa kwa ajili ya watoto wa lika hilo kwenda nje ya nchi na wanakwenda kufanya nini.

“Watoto wengi wamekuwa wakichukuliwa majumbani na kupelekwa kusikojulikana kwa kigezo cha kwenda kutafutiwa ajira, lakini ukijaribu kufuatilia utakuta wengi huishia kupelekwa kwenye majumba ya starehe, na wengine kufanyishwa biashara za ukahaba kwenye maeneo mbalimbali kama kivutio cha biashara za watu kinyume na matarajio na bila ridhaa yao,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Relief Initiatives, Edwin Mugambila alisema hali ni mbaya na kuwa biashara hiyo hivi sasa ipo mikoa yote lakini iliyoathiriwa zaidi ni ile ya pembezoni kutokana na muingiliano wa watu na ndiyo maana wamekuwa wakifanya semina hizo katika mikoa yote ili kuwajengea uelewa wananchi.

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Singida Phaustine Ngunge alisema ili kukabiliana na tatizo la biashara hiyo haramu, pamoja na mambo mengine inahitajika zaidi kutolewa kwa elimu kwa wananchi na sheria ziangaliwe upya.

Dotto Mwaibale na Philemon Mazalla, Singida

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments