SERIKALI HAINA KESI ZA KODI ZA SH. TRILIONI 360

Serikali imesema kuwa haina kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Sh. trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 ambazo hazijaamuliwa katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa la Kodi (TRAT) bali kuna mashauri 854 yaliyo kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji, yenye kodi inayobishaniwa ya jumla ya Sh. trilioni 4.21 na dola za Marekani milioni 3.48.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina, aliyetaka kujua sababu inayofanya kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Shilingi trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 hazijaamuliwa hadi sasa.

Akifafanua kuhusu kiasi cha Sh. bilioni 700 kilichopokelewa na Serikali Mhe. Nchemba alisema kuwa kiasi hicho kilikuwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa baada ya kuundwa timu ya kusimamia makubaliano hayo mwaka 2017/2018 kati ya Serikali na Kampuni ya Barick.

‘‘Makubaliano hayo yaliisha Januari 24, 2020 ambapo Tanzania ilikubali kuachilia Sh. trilioni 360 ili kumaliza shauri lile na kuunda Kampuni ya Twiga ambapo Serikali ina ubia asilimia 16 na Kampuni ya Baricki ina asilimia 84’’, alisema Mhe. Nchemba.

Alisema makubaliano hayo pia yaliifanya Kampuni ya Barick kufuta kesi iliyofungua dhidi ya Tanzania iliyokuwa na madai ya dola za Marekani bilioni 2.7 na kukubaliana Kampuni hiyo itoe dola za Marekani milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na pia kutoa dola 6 kwenye kila dhahabu na dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya madini.

Aidha, Mhe. Nchemba ameeleza kuwa kwa sasa taasisi za rufaa za kodi zinaendelea kusikiliza mashauri hayo pamoja na mashauri mapya yanayoendelea kusajiliwa kwani idadi ya mashauri ya kodi hupungua au kuongezeka kulingana na kasi ya usikilizaji na usajili kwa nyakati tofauti.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments