Serikali Kutengeneza Kanuni za CSR Migodini


Serikali ipo kwenye mchakato wa kutengeneza kanuni na muongozo maalumu utakaofanya migodi ya uchimbaji madini nchini kutekeleza miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) lengo likiwa ni kuwezesha wananchi wanaozunguka migodi kunufaika na utajiri uliopo.

 Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko amesema hayo wakati alipotembelea mgodi wa madini Geita (GGM) na kusema muongozo huo ukikamilika utawezesha kampuni kutekeleza miradi ya CSR bila bila kutegea.

Amesema utaratibu uliopo sasa ni wa migodi yenyewe kuamua cha kufanya jambo ambalo limefanya migodi mingine kutegea huku wakichukua utajiri mkubwa na kuwaacha wananchi wa eneo husika na umaskini.

“Nchi hii kampuni inayofanya vizuri kwenye CSR kwenye madini ya kwanza ni GGM ndio mzalishaji mkubwa lakini hata ile nia ya kushirikiana na wananchi kwa ajili ya kutengeneza miradi ya kimaendeleo GGM wanafanya kazi nzuri sana “

Amezitaka kampuni za uchimbaji pamoja na migodi midogo kutambua wapo wananchi wanaozunguka maeneo yao na wanapaswa kunufaika na utajiri uliopo kwa kuboreshewa huduma za maji, shule na hospitali na sio kuwaacha kwenye umaskini.

“Geita kwa sasa tunachogombana sio hela tuzipate wapi kwa sasa tunaulizana hela tunazitumiaje huko nyuma mika saba iliyopita tulikua hatuzungumzi hili  ni vema na migodi mingine wajue hakuna fahari yoyote ya kuchukua utajiri mkubwa alafu unawaacha wananchi hawana shule,hospitali wala maji ni lazima kurudisha kwa wananchi” alisema Biteko.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti Tanzania na Ghana, Simon Shayo amesema mgodi huo utaendelea kushirikiana na wananchi kutekeleza miradi ya maendeleo na kusema mgodi huo umekuwa ukitoa Sh 9.2 bilioni kila mwaka kwa ajili ya miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR)

Amesema katika kutii agizo la Serikali la kutosafirisha Carbon kwenda nje ya nchi mgodi huo umejenga mtambo kwa ajili ya kuchenjua mabaki ya Carbon yanayotoka kwenye kinu cha kuchenjua dhahabu katika mgodi huo.

“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna dhahabu inayotupwa mtambo huu unachenjua mabaki ya Carbon yanayotoka kwenye kinu cha uzalishaji dhahabu lakini pia dunia kwa sasa ipo kwenye jitihada za kuzuia hewa ukaa na sisi tunaungana na dunia kuhakikisha tunapunguza hewa ukaa kwenye mazingira”alisema Shayo.

Katika hatua nyingine Shayo amesema mgodi huo upo kwenye mradi wa kujenga kinu cha kupoozea umeme kinachojengwa kwa zaidi ya Sh50 bilioni ambapo ukikamilika utapunguza matumizi ya umeme unaozalishwa kwa mafuta kwa zaidi ya asilimia 50.

“Sisi tunajenga kinu lakini pia Tanesco wanajenga njia ya kilomita sita kuhakikisha umeme unafika mgodini mradi huu ukikamilika tunategemea hadi mwezi Machi mwakani tuanze kutumia umeme wa gridi ya Taifa hii itatusaidia kupunguza gharama kwa sasa tunazalisha umeme uniti moja kwa senti 19 lakini kwa Tanesco tutazalisha kwa senti tisa”.amesema Shayo

Mbunge wa Geita mjini, Costantine Kanyasu amesema kilio chake cha muda mrefu ni kutaka ushiriki wa watu wa Geita kwenye uchumi wa mgodi ambapo sasa wanapata nafasi za kutoa huduma ndani ya mgodi na kutaka wananchi wasisite kuomba zabuni pindi zinapotangwazwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments